Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli amekuwa hapati wakati mgumu anapowasilisha bajeti ya wizara hiyo, lakini hali ilikuwa tofauti jana wakati wabunge walipoungana kueleza hofu yao katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara kutokana na madeni ya makandarasi.
Wabunge hao walidiriki kueleza kuwa kuna ufisadi
katika ununuzi wa kivuko cha Bagamoyo na wengine kueleza kuwa miradi
iliyotajwa kwenye hotuba ya bajeti ilishatekelezwa miaka ya 80 na 90.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Miundombinu
kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 iliyosomwa na
Makamu Mwenyekiti, Profesa Juma Kapuya, deni linalodaiwa na makandarasi
ni kati ya Sh850 bilioni na Sh900 bilioni.
“Kamati haijaridhishwa kabisa na hali hii kwani
deni hili sasa ni kubwa kuzidi hata bajeti inayotengwa kwa ajili ya
miradi ya maendeleo ya wizara hii, jambo ambalo linafanya bajeti hii
kuonekana ni kiini macho tu,” alisema Profesa Kapuya.
Kambi ya Upinzani
Katika taarifa yake, Kambi ya Upinzani Bungeni
(KUB) ilimshutumu Waziri Magufuli kwa kuandika hotuba ndefu ili
kuwachanganya wabunge, huku hotuba hizo zikitaja hata miradi ya barabara
zilizojengwa miaka ya 80 na 90.