Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana. Wengine ni wenyeviti wenza, James Mbati, Profesa Ibrahim Lipumba na Dk Emmanuel Makaidi.
Saa 48
zilizotumika kikaoni kutafuta muafaka wa majimbo yenye utata ndani ya
umoja wa vyama vya upinzani vilivyo chini ya Ukawa, zimekatika bila
mafanikio na mvutano unaonekana kubakia kwenye majimbo 12 kati ya 239
waliyopanga kugawana.
Vyama hivyo vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kiti cha urais
hadi udiwani, lakini kazi ya kugawana majimbo imekuwa ikivisumbua na
ilitarajiwa kuwa ingemalizika juzi baada ya viongozi kukutana kwa siku
mbili kuanzia Jumanne.
Lakini habari kutoka ndani ya kikao hicho
kilichofanyika jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa wajumbe walishindwa
kufikia muafaka kwenye majimbo 12.
Hata hivyo, viongozi hao wa vyama hivyo walikataa kutaja majimbo hayo yaliyosalia. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi
za makao makuu ya CUF, viongozi wa vyama vinne vinavyounda Ukawa, James
Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema), Profesa Ibrahim Lipumba
(CUF) na Emmanuel Makaidi (NLD) walisema tayari wamefikia muafaka katika
majimbo 227 kati ya majimbo 239 yaliyopo nchini.
“Tangu juzi tupo hapa tukijadili namna ya kuwapata
wagombea wa Ukawa wa ngazi zote za udiwani, ubunge na urais. Kwa kiasi
kikubwa tumekamilisha kazi ya kupata wagombea ubunge kwa zaidi ya
asilimia 95 ya majimbo yote ya uchaguzi, majimbo 12 yaliyobaki
tunaendelea kuyashughulikia na tutayapatia ufumbuzi muda si mrefu,”
alisema Mbatia aliyezungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake.
Viongozi hao, kila mmoja kwa nyakati tofauti,
walijigamba kuwa umoja wao huo upo imara na kwamba wale wanaopiga ramli
kuwa utavunjika, wataendelea kusubiri lakini kamwe jambo hilo
halitatokea.
Mbowe
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Mbowe alisema
hatua iliyofikiwa kwa sasa inatia matumaini ya kufanikiwa kwa mpango wa
kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge, udiwani na urais.
“Kwa wale wanaopiga ramli ya kuvunjika kwa Ukawa
hawatafanikiwa. Tutasimamisha mwakilishi mmoja kuanzia udiwani, ubunge
mpaka urais. Tunajua hitaji la Watanzania kwa sasa ni kuwaondoa kwenye
kifungo cha CCM,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa kuhusu mvutano wa majimbo hayo 12,
Mbowe alisema siyo jambo la kushangaza kwa vyama vinne kutovutana katika
mgawanyo wa majimbo hayo kwani kila chama kinajiamini na kinahitaji
kupata mwakilishi.
“Tuko vyama vinne, itakuwa ajabu kama mvutano
utakosekana, lakini tumepata asilimia 95. CCM wenye chama kimoja
hawajatangaza mgombea hata mmoja.”
Mbowe alisema madai ya kuchelewa kutangaza wagombea wa Ukawa
katika ngazi za ubunge, udiwani na hata ile kubwa ya urais ni mkakati
wa kisiasa na kwamba watayataja muda muafaka utakapowadiwa.
“Sisi hatutegeani na CCM, muda utakapofika tutawaambia Watanzania,” alisema Mbowe.
Mbowe pia alisema maandalizi hafifu yanayofanywa
katika uboreshaji Daftari la Wapigakura ni mipango wa makusudi
unaofanywa na Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili
kumwongezea Rais Jakaya Kikwete na serikali ya CCM muda wa kukaa Ikulu.
“Miezi mitatu tu imebakia kabla ya kampeni za
uchaguzi, lakini mpaka sasa hatujui ratiba, majimbo yaliyogawanywa,
watumishi watakaotumika, vituo vitakuwaje vya uchaguzi na hata daftari
la kupigia kura ndiyo bado halijamaliza hata mikoa miwili, hiyo ni
hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC isijaribu kufanya mbinu
zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu,”
alisema Mbowe.
Mbatia
Kwa upande wake, Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, alisema ahadi na kauli za NEC zimekuwa na utata hali
inayowafanya waondoe uaminifu kwa Tume hiyo.
Mbatia alisema mpaka sasa kuna mashine 1,100 tu za
BVR kati ya mashine 8,000 zinazotakiwa kuingia nchini kwa ajili ya
kufanyia kazi.
Alisema tathmini waliyofanya inaonyesha kwamba,
endapo kila kituo kitatumia siku 14 za uandikishaji wa wapigakura, yaani
vituo 40,000, zoezi hilo litatumia siku 353, sawa na mwaka mmoja.
“Kwa sasa kati ya Watanzania milioni 24
wanaotakiwa kuandikishwa kwenye daftari hilo, ni Watanzania chini ya
200,000 tu ndiyo walishaandikishwa huku miezi iliyobakia ikiwa ni mitatu
tu,” alisema Mbatia.
Kuhusu mpango wa kufanyika Uchaguzi Mkuu na Kura
ya Maoni kwa wakati mmoja, Mbatia alisema jambo hilo haliwezekani kwa
mujibu wa Katiba, na kuwa kura ya maoni inayo sheria yake na mpaka sasa
sheria hiyo tayari imevunjwa na NEC.
“Kwa hivyo tunaitaka NEC itamke kusitisha mpango
wake wa kuunganisha matukio hayo mawili, lakini pia itoe tamko la
kufanyika Uchaguzi Mkuu kama ilivyo kawaida kikatiba,” alisema.
Hata hivyo, tayari NEC imeshaeleza kuwa itakuwa
vigumu sana kufanya mambo hayo mawili kwa wakati mmoja kwa kuwa kila
tukio lina mahitaji yake tofauti.
Profesa Lipumba
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
NEC, haijaanza maandalizi yoyote licha ya kubakia miezi sita tu kabla
ya Uchaguzi Mkuu na kuongeza kuwa wamebaini zipo njama za kuuahirisha
ili kumuongezea muda Rais Kikwete na CCM.
Profesa Lipumba alisema kwa Sheria ya Kura ya
Maoni, hakuna uwezekano wa jambo hilo kufanyika tena bila kwanza kufanya
marekebisho ya sheria hiyo.
Alisema Kura ya Maoni ilitakiwa ifanyike ndani ya
siku 124 kutoka tarehe Rais Kikwete alipotoa tangazo la kura ya maoni
pale alipotamka kuwa kura hiyo itafanyika 30 Aprili 2015.
“Kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa chini ya
sheria hiyo imewekewa muda wake na muda huo hautakiwi kubadilika...
tangazo la Kura ya Maoni likishatolewa na tarehe kutangazwa,
haibadilishwi kwa sababu yoyote ile. Hivyo hakuna namna yoyote ya
kuahirisha Kra ya Maoni na kuifanya tarehe nyingine yoyote” alisema
Lipumba.
Dk Makaidi
Mwenyekiti wa NLD, Dk Makaidi alisema zipo dalili
na ushahidi kuwa uchaguzi ukifanyika mwaka huu CCM itang’olewa
madarakani na kwa kulijua hilo, Serikali inafanya kila njia ili
kuahirisha uchaguzi usifanyike mwaka huu.
“Kubadili Katiba ya sasa kwa lengo la kuahirisha
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu sio tu kutaathiri misingi muhimu ya
Katiba ya sasa, bali pia kutaathiri amani ya nchi yetu. Tumeona
kinachoendelea Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunzinza na chama chake
kuamua kujiongezea muda wa kutawala nchi hiyo,” alisema.
“Tumeona yanayoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Conga (DRC) baada ya Joseph Kabila kutaka kufanya hivyo, Kikwete na
wana-CCM wenzake wasitake kuiingiza nchi yetu katika majanga yasiyokuwa
na sababu,” alisema.
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment