Yanga imeendelea kutoa
dozi Ligi Kuu Bara baada ya kuichapa 2-1 JKT Ruvu katika mechi
iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa huku Mtibwa Sugar ikiichapa
Mgambo Shooting 1-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro na kujikita
kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Hii ni mechi ya pili kwa Yanga kushinda katika
Ligi Kuu kwani iliichapa Tanzania Prisons 2-1, lakini katika mechi yake
ya ufunguzi wa msimu huu ilichapwa 2-0 na Mtibwa hivyo kuanza safari
yake ya kusogea katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi kwa mwendo
mdogo mdogo.
Katika mechi ya jana, hadi mapumziko Yanga ilikuwa
ikiongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa kwa shuti kali na beki Kelvin
Yondani dakika ya 35 akiunganisha pasi safi ya Haruna Niyonzima.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Niyonzima kwa
mpira wa faulo uliokwenda moja kwa moja nyavuni dakika ya 73 huku bao la
JKT Ruvu likifungwa dakika ya 90 kwa shuti kali na Jabir Aziz akiwa nje
ya 18. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz