Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema
atafurahi kuona mchakato mzima wa Katiba ukikamilika kabla rais mpya
hajapatikana katika Uchaguzi Mkuu ujao, pendekezo ambalo ni kinyume na
makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) kuwa upigaji wa kura ya maoni ufanyike baada ya Uchaguzi
Mkuu 2015.
Akizungumza Bungeni baada ya kupewa nafasi na
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kutoa shukrani, Pinda
alipendekeza kura ya maoni ipigwe sambamba na Rais ili kiongozi ajaye
afanye kazi ya kutekeleza matakwa ya Katiba hiyo.
Alisema rais ajaye anaweza kuwa na ajenda zake,
hivyo ni muhimu kumaliza kazi yote na kumkabidhi Katiba ambayo
imekamilika ili aitekeleze.
“Nampongeza sana mwenyekiti kwa kufanya kazi nzuri
ya kuhakikisha Katiba inayopendekezwa inapatikana kwa wakati na kwa
kuzingatia maoni ya wananchi,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Alichojifunza
Pinda alieleza kuwa katika mchakato huo wa
Mabadiliko ya Katiba, amejifunza mambo makuu manne, kubwa likiwa ni
kutii sauti ya wengi, kwani ni sauti ya Mungu. Alisema wingi wao bungeni
ni kiashiria cha uwepo wa sauti ya Mungu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Alisema umoja wao bungeni ni silaha muhimu
iliyofanikisha hatua zote zilizowezesha kupatikana kwa Katiba
inayopendekezwa, bila kujali pingamizi kutoka kwa watu waliojaribu
kukwamisha mchakato huo.
“Nawaomba sasa kwa umoja wetu huu, twende nao kwa
wananchi ili kueleza kuwa kazi waliyotutuma tumeikamilisha na wao
watuunge mkono katika kura ya maoni,” alisema.
Alisema amevutiwa zaidi na Sura ya Pili ya Katiba
hiyo kwa sababu imechukua malengo makubwa ya kitaifa katika nyanja za
kiuchumi, kisiasa na kisera. Aliwapongeza Wazanzibari akisema wasiwasi
wa wengi ulikuwa kukosekana kwa theluthi mbili kutoka kwa wajumbe wa
upande huo wa pili wa Tanzania. “Nimetambua kuwa wote wanajenga Taifa
moja na wao ni wamoja,” alisema.
Ulinzi na usalama
Pinda alisema suala la ulinzi na usalama ni ajenda
ya Taifa hili na kwamba anashangaa kuona baadhi ya watu wakikaa na
kupanga kuvuruga amani ya nchi kwa masilahi binafsi.
Alisema maridhiano ndiyo njia pekee inayoweza
kuleta suluhu baina ya pande mbili zinazotofautiana kimawazo na siyo
kwenda kufanya vurugu kama wafanyavyo baadhi ya wajumbe waliosusia Bunge
hilo.
Bunge lahitimishwa
Akihitimisha Bunge hilo Mwenyekiti wake Samuel
Sitta, alisema Rais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohammed Shein wamekubali
kuwa shughuli ya kuzipokea Katiba ifanyike Jumatano ijayo.
“Watapokea nakala ya Katiba inayopendekezwa hapa
Dodoma katika sherehe maalumu,” alisema na kuongeza kuwa Rais pia
amekubali kila aliyeshiriki mchakato huo na kufikia mwisho atapewa
cheti.
Sitta pia alizishukuru kamati zote 12 zilizohusika
katika kuboresha Rasimu na kutengeneza Katiba inayopendekezwa ambayo
alisema imebeba maoni ya wananchi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Walichosema wengine
Baadhi ya wajumbe waliopewa nafasi ya kuzungumza
wamewapongeza viongozi wa Bunge la Katiba; Mwenyekiti, Samuel Sitta na
Makamu wake Samia Suluhu Hassan, pamoja na Kamati ya Uandishi
iliyoongozwa na Andrew Chenge kwa kufanya kazi hiyo ngumu, bila kujali
walivyoshambuliwa.
Mjumbe Hamad Rashid alisema kuna baadhi ya watu
walisema wao wana kura za Wazanzibari na kuwa walipendekeza Serikali ya
mkataba. Hata hivyo, alisema, matokeo yaliyotolewa ndiyo yamebainisha
nani ni Wazanzibari na Serikali gani wanaitaka.
“Katiba inapatikana kisheria, ndiyo maana tumekuwa
hapa kuifanya kazi hiyo. Sasa hawa wenzetu waendelee kupiga kelele
wenyewe. Sasa ni wazi kuwa sauti ya watu wa Kibanda Maiti imesikika
katika matokeo haya,” alisema Rashid.
Mjumbe mwingine, Stephen Wasira alisema: “Wapo
waliosema wao ndiyo wanawasemea wananchi lakini waliondoka humu ndani
sasa wanakwenda kusemea wapi. Wengine wakasema tutakutana mtaani sawa,
tutakutana huko maana ndiko tunakoishi,” alisema Wasira.
Aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo, Pandu
Ameir Kificho aliwapa pole Sitta na Samia kwa kupitia changamoto nyingi
kuliko ilivyokuwa wakati wake.
Alisema anakumbuka wakati wake alizushiwa kuwa
anarefusha mjadala wa kuandaa kanuni ili ajikusanyie fedha nyingi za
posho ya Sh7 milioni kwa siku, jambo ambalo alikanusha na kusisitiza
kuwa alilipwa posho kama wajumbe wengine.
Mjumbe John Shibuda alisema hakutaka kuwa sehemu
ya wasaliti ndiyo maana alishiriki kikamilifu katika kutengeneza
historia ya Taifa. Alisema ni heri kuitwa msaliti kuliko kuwa mhaini wa
Watanzania.\
Na Mwananchi
Askofu Donald Mtetemela alipinga matamko yaliyotolewa kwenye
vyombo vya habari kuwa hayakuwa ya maaskofu kwa sababu hayakusainiwa na
maaskofu wote kama ambavyo hufanyika mara zote wakitoa tamko.
Alisema yalikuwa maoni ya mtu binafsi na si maoni
ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) au Makanisa ya
Kipentekoste (PCT). Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment