Dodoma/Dar. Licha ya upinzani kutoka makundi
kadhaa ya wananchi, Bunge la Katiba jana lilihitimisha kazi yake kwa
kupitisha Katiba inayopendekezwa baada ya kupata theluthi mbili za
wajumbe wa kila upande wa Muungano.
Matokeo hayo yaliyohitimisha mchakato huo,
yalifanikishwa kwa tofauti ya kura mbili za wajumbe katika baadhi ya
ibara na nyingine kwa kura moja tu, ikimaanisha kuwa iwapo kura hizo
mbili zingekosekana hadithi ingekuwa tofauti.
Kutangazwa kwa matokeo hayo kuliwafanya wajumbe
walioshiriki mchakato hadi hatua ya mwisho baada ya wenzao wa kundi la
Ukawa kususia, kulipuka kwa furaha, nyimbo, tambo, vijembe na vigelegele
huku wakijimwaga ukumbini kusakata dansi.
Akitangaza matokeo hayo, Naibu Katibu wa Bunge
hilo, Dk Thomas Kashililah alisema hali ya upigaji kura ilikuwa ni nzuri
na kila kura za kila upande zilitosheleza na kutoa uhalali wa Katiba
inayopendekezwa kupelekwa kwa wananchi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Katibu huyo alianza kutoa matokeo ya upande wa
Zanzibar ambako wajumbe wengi walikuwa na wasiwasi kuwa huenda usipate
akidi ya kura 146 iliyotakiwa.
Kwa jumla, kura za ‘ndiyo’ za Zanzibar zilikuwa
ama 147 au 148 na ‘hapana’ ama saba au nane; wakati kwa matokeo ya
Tanzania, wajumbe waliopiga kura walikuwa 335 na kura moja tu ndiyo
ilikataa ibara zote na kura mbili zilichomoza kukataa baadhi ya ibara.
Matokeo hayo yalithibitishwa na mawakala Amina
Makilagi na Waziri Rajabu Salum ambao walisimama na kueleza namna
ambavyo kura hizo zilihesabiwa kwa uhuru mpana.
Kuserebuka bungeni
Baada ya matokeo hayo, Ukumbi wa Bunge
ulihanikizwa kwa nyimbo za mipasho na mafumbo zikiambatana na kuwashwa
vipaza sauti bila ya utaratibu na wajumbe kurukaruka na kukumbatiana kwa
furaha.
Hali hiyo, iliwalazimu walinzi wa viongozi kuingia
ndani ya ukumbi kwa kuweka hali ya amani kwani wajumbe walianza kuvamia
viti vyao kwa nia ya kuwapongeza.
Hali ilipozidi, walinzi wa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda walimwondoa haraka na kumweka katika chumba maalumu hadi hali
ilipotulia huku idadi kubwa ya walinzi ikisogea kwa Mwenyekiti wa Bunge,
Samuel Sitta.
Baada ya kuwatuliza, Sitta alisema walichokuwa wanafanya ni
kuvunja kanuni, lakini kwa kuwa mwenyekiti naye alikuwa akicheza basi
hakuna tatizo na amewasamehe.
Filikunjombe, Lugora wakwama
Wabunge wawili, Deo Filikunjombe (Ludewa- CCM) na
Kangi Lugola (Mwibara-CCM) ambao hawakuwapo wakati wa mchakato, jana
waliingia ukumbini lakini Sitta alitangaza kuwa haikuwapo tena nafasi ya
kupiga kura.
“Nitangaze leo kuwa hakuna nafasi ya kupiga kura
kwa wajumbe ambao hawakupata nafasi hiyo, nasema hivyo kwa kuwa matokeo
yote tunayo hapa na hivyo hakuna sababu za kupiga kura tena,” alisema
Sitta.
Wakati wa upigaji wa kura, majina ya wabunge hao yalipoitwa wajumbe waliitikia kwa sauti “ukawa haooo”.
Baada ya tangazo hilo, wabunge hao waliamua
kuondoka ukumbini na kutokomea. Lugola hakupatikana kwa simu kuzungumzia
hali hiyo lakini Filikunjombe alipokea simu na kusema alikuwa kwenye
mkutano.
Ukawa: Harakati kuendelea
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema
harakati za kuipata Katiba bora yenye masilahi ya wananchi zitaendelea
bila kusimama.
“Tumeona kichekesho na dhihaka iliyotokea Dodoma,
kwa mustakabali wa Taifa hili. Ni vyema CCM wakawa makini kutotumia
vibaya fursa hii ya kuiongoza nchi kwa kuzingatia hoja na matakwa ya
kuipata Katiba, bila kutumia rushwa wala nguvu ya dola.
“Bado tunajadiliana ili tutoe tamko la pamoja.
Rasimu iliyopitishwa ina maswali mengi kuliko majibu. Baada ya muda
mfupi wa kujadiliana baina yetu tutasema msimamo wetu,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Profesa Issa Musoke alisema wananchi hawana sababu ya kuikubali rasimu
iliyopitishwa kwa kuwa ni batili. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Rasimu iliyopitishwa ni ya kamati ya uandishi na
siyo ya Taifa hili kwa sababu imekiuka kanuni. Rais aliunda Tume ya
kukusanya maoni ya wananchi ambayo yangejadiliwa katika Bunge Maalumu la
Katiba, kama taratibu zilivyoainisha. Bunge hilo lilikuwa na jukumu
moja la kutunga Katiba kutokana na maoni ya wananchi,” alisema na
kuongeza:
“Watanzania tumekuwa waoga wa kupitiliza. Hatutaki kusema ukweli
hata kama unahitajika. Kwa kilichofanyika ni kwamba wananchi
hawakutendewa haki.”
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Humphrey Polepole alisema wajumbe wanafurahia kupitisha Katiba
inayopendekezwa katika mazingira ya kushindwa.
“Wameshindwa kutupatia Katiba inayotokana na maoni
ya Watanzania. Wametoa maoni ya wananchi na kuweka yao. Huwezi kupata
Katiba nzuri kama hakuna maridhiano huku mijadala yote ikitawaliwa na
itikadi za vyama vya siasa na mizengwe,” alisema.
Alisema kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kupiga kura ya
‘hapana’ kinaonyesha kuwa Zanzibar imegawanyika zaidi na hilo
lilidhihirika baada ya mwanasheria huyo kutaka kupigwa na wajumbe
wenzake kutoka huko.
Alisema wajumbe wa Tume hiyo wataendelea kuitetea
Rasimu ya pili ya Katiba iliyotolewa na Tume hiyo kwa sababu ilitokana
na maoni ya wananchi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya
Ardhi (HakiArdhi), Yefred Myenzi alisema Katiba inayopendekezwa ni
kichekesho kwa sababu licha ya kupingwa na wananchi wengi, imeongezwa
sura mpya ya ardhi ambayo haijajibu mambo manne ya msingi kuhusu ardhi.
Alitaja mambo yaliyokosekana katika sura ya ardhi
iliyoongezwa kuwa ni; kutoeleza ardhi inamilikiwa na nani, vyombo vya
kusimamia ardhi, mfumo wa matumizi ya ardhi na uhusiano kati ya ardhi na
rasilimali nyingine.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema,
“Zoezi la upigaji kura lilikosewa na lilikosa uwazi, hasa kwa wajumbe
waliopiga kura kwa njia ya faksi na baruapepe. Ilitakiwa tuelezwe idadi
yao kamili pamoja na majina yao ili kujiridhisha kama kweli kura hizo
siyo za maruhani.”
Aliongeza, “Kwa kutumia vyanzo vyangu nilifanikiwa
kuona kura ya mmoja wa wajumbe waliopiga kwa njia ya mtandao. Kwa jinsi
ilivyokuwa, ilikuwa rahisi kwa kura hizo kuchakachuliwa.”
Dk Slaa aliponda kitendo cha wajumbe wa Bunge hilo
wakati wakipiga kura, kutamka kuwa wanapiga kura kwa niaba ya kundi
fulani kwa sababu kitendo hicho ni kinyume na kanuni za uchaguzi ni sawa
na kufanya kampeni.
“Wajumbe wa Bunge la Katiba pia walikosea sana
kusema kuwa Katiba iliyopendekezwa imetambua haki za makundi yote bila
kuwaeleza wananchi kuwa Ibara ya 20 ya Rasimu ya Katiba inakataza haki
hizo kudaiwa mahakamani,” alisema.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustine (Saut), Dk Charles Kitima alisema: “Katiba inayopendekezwa ina
uhalali wa kisheria lakini inakosa uhalali wa wananchi.
Na Mwananchi
“Haikuwa busara kupuuza maoni ya wananchi na Tume ya Katiba.
Katiba hii imepitishwa kwa ubabe wa CCM na watu watambue kuwa siku
wananchi wakipata fursa ya kujitawala kidemokrasia wataidai Katiba yao
tu.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence
Mpangala alisema: “Jambo la msingi si kupata theluthi mbili ya wajumbe
kupitisha Katiba. Katiba lazima ipatikane kwa maridhiano na si kwa ubabe
kama ilivyotokea Dodoma.
“Unaweza kutumia ubabe katika hatua ya kupiga kura
kupitisha Katiba inayopendekezwa, lakini huwezi kutumia ubabe huo
katika upigaji wa kura ya maoni. Tangu mwanzo nilipinga mchakato huu kwa
sababu watu waligawanyika na ilitakiwa maridhiano yafanyike kwanza.”
Profesa wa Sheria UDSM, Chris Peter Maina alisema:
“Utaratibu uliotumika utawagawa wananchi. Katiba haipatikani kwa namba,
bali kwa maridhiano. Siombei mabaya lakini ukweli ndiyo huo, hii Katiba
itatugawa na si jambo la kushangilia hata kidogo.”
Alisema Katiba inayopendekezwa ni dhaifu kwa
sababu haina maoni ya msingi yaliyotolewa na wananchi ambayo yalikuwa
katika rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo kwa
miezi 20 ilifanya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi.
Wakili Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema: “Nina uchungu sana kwa sababu
kwa mara nyingine Tanganyika tumeizika. Hata hivyo, LHRC tunafanya
tathmini ya mchakato mzima wa Katiba na tutatoa tamko rasmi.” Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment