Rais Jakaya Kikwete ametakiwa kufuta
kauli yake ya kuwataka wana CCM kuacha unyonge na kujibu mapigo dhidi ya
upinzani na ametakiwa kuomba radhi ndani ya siku tatu, vinginevyo suala
hilo litafikishwa jumuiya za kimataifa.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati
wa kufunga Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho Mjini Dodoma
mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo Chadema wanaitafsiri kama kielelezo
cha kuvuruga amani ndani ya nchi.
Kwa majibu CCM kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kamwe hawatafanya hivyo.
"Kauli aliyoitoa Rais Kikwete ni ndogo
na kutokana na vitendo vinavyofanywa na viongozi na wanachama wa
Chadema kuvuruga amani nchini," alisema na kuongeza kuwa dawa ya moto ni
moto.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa
Chadema, Benson Kigaila alisema kuwa Rais Kikwete anatakiwa kufuta
alichokizungumza ndani ya siku tatu kuanzia jana, vinginevyo
watalifikisha suala hilo mbele ya jumuiya ya kimataifa kama sehemu ya
malalamiko yao.
Alisema kuwa Rais Kikwete ni Amiri
Jeshi Mkuu, na alihoji kwanini awatake WanaCCM kujibu mapigo dhidi ya
wapinzani badala ya kuacha hatua za kisheria zikafuatwa kwa kutumia
vyombo husika ambavyo ni polisi na majeshi na mahakama. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz
Chanzo:Mwananchi