RAIS Jakaya Kikwete amemshangaa Mwenyekiti wa Simba SC ya jijini Dar es Salaam, Ismail Aden Rage kwa kuitisha mkutano wenye ajenda moja kwa ajili ya wanachama wa klabu hiyo. Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Simba Rage, alitangaza kuwepo kwa mkutano wa klabu hiyo Machi 23 na kueleza wazi kuwa kutakuwa na ajenda moja ya kujadili mapungufu ya Katiba.
Akizungumza mbele ya umati wa watu
waliohudhuria mazishi ya Mbunge wa Chalinze, Saidi Bwanamdogo mwishoni
mwa wiki iliyopita, Rais Kikwete ambaye alifika katika eneo la makaburi,
alimuuliza Mwenyekiti huyo wa Simba kuhusiana na maandalizi ya mkutano
huo.
"Ndugu yangu Rage mimi Mwenyekiti
mwenzio, lakini sijawahi kuona mkutano wenye ajenda moja ndio kwanza huo
wa kwako, yaani wewe kiboko, pamoja na makelele yote lakini umeweza
kutuliza hali ya mambo mpaka leo umedumu kuwa mwenyekiti," alisikika
Rais Kikwete akisema huku mamia ya waombolezaji wakicheka.
Akizungumzia kauli hiyo ya Rais
Kikwete, Rage alisema ili kuwa kiongozi imara ndani ya klabu za Simba na
Yanga, inakupasa kuwa na roho ngumu, kwani bila ya kufanya hivyo
wanachama watakuwa wakikuchezea kila kukicha.
"Mheshimiwa Rais kuwa kiongozi ndani
ya klabu hizi mbili kunahitaji umakini sana, kwani bila ya kufanya hivyo
wewe utakuwa ni kiongozi wa kupelekwa kila siku na hatimaye unamaliza
muda hakuna ulichokifanya ndani ya uongozi wako," alisema Rage. Chanzo:
mtanzania