ALIYEKUWA Mlinzi mkuu (bodyguard) wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame,
Luteni Joel Mutabazi, ametekwa na kikosi cha Jeshi la Uganda na
kukabidhiwa kwa Serikali ya Rwanda.
Taarifa za kiintelijensia zinasema
kuwa Luteni Mutabazi, alikuwa akiishi nchini Uganda kwa hati maalumu ya
ukimbizi ya Umoja wa Mataifa, baada ya kutoroka nchini Rwanda pamoja na
aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, Faustin Kayumba Nyamwasa.
Luteni Mutabazi alitorokea nchini Uganda Oktoba 2011, baada ya kutoroka jela yenye ulinzi mkali wa kijeshi ya Kami nje kidogo mwa mji wa Kigali akituhumiwa kwa kuhusishwa na kutoroka kwa mkuu huyo wa majeshi na kukimbilia Afrika Kusini. Alikuwa mlinzi mkuu wa Rais Kagame mpaka mwaka 2010, alipotoroka na kukimbilia Uganda.
Mlinzi huyo pia anashutumiwa na Serikali ya Rwanda kwa kutoa siri kwa Kikosi Maalumu cha Umoja wa Mataifa chini ya Majeshi ya Umoja ya Kulinda Amani nchini Kongo, (MONUSCO) na kuwezesha kuchakazwa na kushindwa kwa kikosi cha waasi wa M23.
Kutokana na tukio hilo, hivi sasa Serikali ya Rais Yoweri Museveni, imelazimika kumsimamisha kazi Mkuu wa Intelijensia wa Jeshi la Polisi, Joel Aguma, ambaye alihusika kumteka na kumkabidhi Luteni Mutabazi kwa Serikali ya Rwanda.