Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi
wa kupata Kamati mpya ya Utendaji ya shirikisho utafanyika Oktoba 27
mwaka huu kama ilivyopangwa.
"Wazungu wanasema ije mvua au jua,
uchaguzi utafanyika. Isipokuwa tunachotaka kuhakikisha ni kuwa unakuwa
uchaguzi huru na wa haki," amesema Rais Tenga wakati akizungumza na
waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana (Oktoba 7 mwaka huu).
Amesema mchakato unakwenda vizuri
kilichobaki ni revision (mapitio) na rufani, masuala ambayo yako mbele
ya Kamati ya Rufani ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi.
Rais Tenga amesema lengo la hatua hizo
si kuzuia watu wasigombee kwani ni lazima mambo ya msingi ikiwemo sifa
za wagombea yaangaliwe, lakini kwenye haki ni lazima kuhakikisha
inatendeka hata kama ni kwa mtu mmoja.
Mchakato wa uchaguzi ulivutia waombaji
58 ambapo watatu wamekata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kupinga
kuondolewa na Kamati ya Uchaguzi wakati wengine wanane masuala yao
yamepelekwa Kamati ya Rufani ya Maadili kwa njia ya mapitio (revision)
ili kupata mwongozo wa utekelezaji.