Valence Robert, Geita
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida kaburi ambalo alizikwa mtoto Shabani Maulidi (15), ambaye anadaiwa kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kuonekana akiwa hai hivi karibuni, jana lilifukuliwa na viungo vya mwili wake kukutwa ndani.
Kazi hiyo iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi pamoja na Mtafiti wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Lucas Ndungulu, ilizua taharuki kwa umati wa watu waliokuwa eneo hilo, baada ya nyumba ya jirani lilipo kaburi hilo, Masanja Marwa, kubomoka ghafla wakati ufukuaji huo ukiendelea, huku mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja naye akianguka na kuzirai.
Kwa sasa mtoto huyo ambaye alionekana hai, amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uangalizi wa kitaalamu.
Akizungumza
na waandishi wa habari eneo la tukio, Ndungulu alisema kuwa wameamua
kufukua kaburi hilo ili kupata sehemu ya viungo vya mwili kwa ajili ya
vipimo.
"Lengo la
kufukua kaburi hili ni kutaka tupate kiungo chochote cha mwili wa
marehemu ili tufanye utafiti wa kitaalamu ili tujue kama ni kweli huyu
anayedaiwa kuwa ni mtoto wao ndiye," alisema.
Alisema
kuwa ufukuaji huo umemalizika na kwamba wamepata baadhi ya viungo vya
mwili wa marehemu na kuchukua baadhi ya mifupa ya mapaja yote mawili
ambayo itapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi
zaidi.
Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote la kukatika kwa umeme.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.
Kwa mujibu wa Ndugulu, majibu ya vipimo hivyo yatatolewa baada ya wiki mbili kama hakutakuwa na tatizo lolote la kukatika kwa umeme.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Adamu Sijaona, alisema kuwa pamoja na kuchukua viungo hivyo, pia watachukua damu ya wazazi na mtoto mwenyewe.
"Tumechukua
pia damu ya mama na baba wa Maulidi mwenyewe ili tukapime vinasaba
(DNA) na kama alivyosema mtafiti, majibu yatatoka baada ya wiki mbili,"
alisema.
Akizungumza
baada ya kazi ya ufukuaji kumalizika, baba mzazi wa mtoto huyo, Maulidi
Shabani, alisema kuwa endapo majibu yatakuja tofauti au vile
wanavyokusudia, wapo tayari kuyapokea na kwamba ikigundulika huyo
aliyeonekana ni Maulidi, pia watampokea na kuendelea kumtunza.
"Lakini nina imani kuwa huyu aliyeonekana ni mwanangu Maulidi kabisa, kwa sababu anazo alama zote," alisema mzazi huyo.
Mtoto
Maulidi aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita na kufanyiwa matanga,
alionekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa ana mapema
wiki hii asubuhi wakati akienda kwenye shughuli zake za biashara.
Ilidaiwa
na wazazi wake kuwa Maulidi alitoweka ghafla na kushindwa kurudi
nyumbani kwao Januari mosi 2011, wakati alipokuwa amewapeleka mbuzi
malishoni na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye
kisima cha maji.
Kwa
mujibu wa baba yake, Maulidi hakurudi nyumbani siku hiyo, ambapo
waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu
walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji
cha Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.
Tukio
hili ni la tatu kutokea mkoani hapa ambapo wilayani Kasamwa, mwanamke
aliyefariki dunia miaka mitano iliyopita alionekana hai na kutambuliwa
na ndugu yake. Tukio la pili lilitokea Wilaya ya Chato, wakati kijana
aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita alionekana akiwa hai.
No comments:
Post a Comment