Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu amesema hotuba ya kila mwezi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa siku tatu zilizopita, imejaa maneno mengi ya kuambiwa hasa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, ikiwa ni pamoja na uteuzi alioufanya wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu wa Chadema, Lissu alisema kauli zilizotolewa na Rais za kumshutumu yeye (Lissu) kuzungumza uongo bungeni, kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba zilikuwa zakuambiwa, hazina ukweli wowote.
"Pengine rais Kikwete angesoma hotuba yangu niliyoitoa bungeni asingezungumza vile kuhusu mimi."
Katika hotuba yake, Rais Kikwete
alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kuwa Rais hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alisema kauli hiyo ya
Lissu ni uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu huku akisisitiza kuwa
Lissu alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga
hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Katika maelezo yake ya jana, Lissu
alisema kuwa alipinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge la Katiba kwa sababu
hata wakati akiteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya
kupelekewa majina na taasisi mbalimbali, alifanya uteuzi wa watu ambao
hawakupendekezwa na taasisi mbalimbali, ikiwemo TEC na CCT.
Lissu ambaye ni mjumbe wa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala alisema kamati hiyo ilipokutana na wawakilishi
wa TEC na CCT (majina yanahifadhiwa kwa kuwa hatukuwapata kuthibitisha
hilo), wawakilishi hao walikiri wazi kuwa majina waliyoyapendekeza sio
ya watu walioteuliwa na Rais.
"Sasa hapo uongo na uzandiki wangu ni
nini, labda hao wawakilishi wa TEC na CCT walisema uongo, hata
wawakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania nao waliieleza
kamati kuwa majina waliyoyapendekeza, sio ambayo Rais aliteua" alisema
Lissu.
Alisema kuwa Rais amemshutumu bila
kuujua ukweli, kusisitiza kuwa kama angesoma hotuba yake aliyoisoma
katika mkutano wa 12 wa Bunge, asingezungumza maneno hayo dhidi yake.
"Ndio maana katika hotuba yake rais
Kikwete alikiri wazi kwa kusema, nimeambiwa, nimesikia, nimeelezwa
ukweli ni kwamba wasaidizi wake wamemdanganya," alisema Lissu.
Chanzo>Mwananchi
No comments:
Post a Comment