HALI ya mambo imezidi kuwa tete katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya Tanzania na Burundi kutaka maelezo ya kina kutoka kwa nchi nyingine tatu wanachama za Kenya, Uganda na Rwanda zilizoanzisha ushirikiano mpya kinyemela kati yao, kwa kuzitenga nchi hizo mbili.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria kuwa Tanzania na Burundi zimetengwa na nchi hizo tatu ambazo zimeanzisha ushirikiano mpya kati yao kinyemela, kinyume cha mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo mwaka 1999.
Jumuiya ya sasa ilizaliwa tena upya Novemba 30, mwaka 1999 ikishirikisha nchi za Tanzania, Uganda na Kenya, wakati Rwanda na Burundi zilikaribishwa baadaye mwaka 2008.
Jumuiya hiyo mpya ilizaliwa baada ya ile ya awali iliyoanzishwa mwaka 1968 kuvunjika mwaka 1977 kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kushindwa kuelewana kwa wakuu wa nchi wanachama kwa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Jommo Kenyatta (Kenya) na Idd Amin (Uganda).
Habari za hivi karibuni zilizopatikana kutoka ndani ya EAC zinabainisha kwamba Tanzania na Burundi zimekerwa na hatua ya nchi wanachama wenzao za Kenya, Uganda na Rwanda kuanza mchakato wa kuanzisha shirikisho la kisiasa bila ya kuzishirikisha nchi hizo.