Na Mwandishi Wetu
MBIVU na mbichi sasa zinaweza
kujulikana, kinachoombwa ni muda tu, kwani mng’amuzi halisi kuhusu kifo
tata cha mwanamuziki mwenye kipaji kikubwa Bongo, Albert Mangwea
‘Ngwea’, yupo kwenye mazingira mazuri kueleza kilichotokea.
KWA NINI ANA USHAHIDI WOTE?
Mwanamuziki
wa Bongo Fleva, Mgaza Pembe ‘M2 The P’, ndiye mwenye ushahidi wote
kwani aliambatana na Ngwea kila sehemu waliyotembelea mpaka nukta ya
mwisho nchini Afrika Kusini.
M2
The P, alipatwa na matatizo sawa na marehemu Ngwea, isipokuwa mwenzake
ilifikia hatua mbaya na kupoteza maisha huku yeye akibaki mahututi
kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) katika
Hospitali ya St. Helen Joseph, jijini Johannesburg nchini humo.
Jambo
la faraja ni kwamba, M2 The P yupo vizuri kwa sasa, atakaporuhusiwa
kutoka, atajibu maswali mengi tata ambayo yamejitokeza tangu Ngwea
alipofariki dunia Juni 28, mwaka huu, nchini humo alipokwenda kwenye
shughuli zake.
JAWABU LA SUMU
Moja
ya mambo yanayozungumzwa pembeni ni kwamba kuna uwezekano mkubwa
marehemu Ngwea na M2 The P waliwekewa sumu kwenye chakula au
kupuliziwa ‘laivu’ kisha kutokea yaliyotokea, lengo likiwa kuwadhulumu
mzigo wa fedha nyingi waliokuwa nao, hivyo kupona kwa mmoja huyo ni
matakwa ya Mungu ili awe shahidi namba moja wa kifo cha Ngwea.