Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako
Dar es Salaam. Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato
cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za
viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.
Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema
matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha
ufaulu kupanda na kufikia
asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale
ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo
hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la
nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na
huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao
82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali
sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.