Waziri
wa Ujenzi Dkt. John Magufuli.
Wizara
ya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imewafukuza kazi na
kusitisha mikataba ya Wafanyakazi Waandamizi saba wa Wizara na Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA) kwa tuhuma za ubadhilifu na utendaji kazi mbovu.
Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Wizara ya Ujenzi ya kusafisha Wakala
zake na kuongeza ufanisi.
Katika
nyakati tofauti Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi amekuwa akipokea tuhuma za
vitendo vya ubadhilifu miongoni mwa watendaji waandamizi katika Wakala
zinazotoa huduma chini ya wizara hii. Kufuatia tuhuma hizo Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi maalum katika
ofisi za TBA Mkoa wa Dar es salaam na Katibu Mkuu wa wizara Balozi
Herbert E. Mrango na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Elius Mwakalinga
waliunda Kamati za kupitia taarifa za CAG na taarifa nyingine. Kamati
hizo zimeweza kubaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za fedha,
manunuzi na uendeshaji.
Maafisa
waliofukuzwa kazi ni pamoja na Bw. Charles Gabriel Lyatuu ambaye
alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa Dar es Salaam; Bw. Ladislaus I. Kapongo
aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa Dar es Salaam) na Bi. Agness F.
Chambo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa Dar es Salaam). Aidha,
kwa Mkurugenzi wa Biashara na Fedha Bibi Yona Orida na Injinia Charles
Makungu ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Miliki wameondolewa katika
nafasi za uongozi walizokuwa nazo TBA.
Hatua
zaidi zilizochukukuliwa ni kuwashusha vyeo Meneja wa Mkoa wa Pwani Bibi
Esteria M. Nyamhanga na Bw. Samwel C. Samike ambaye alikuwa ni Meneja
wa TBA mkoa wa Mbeya.
Hatua
hizi zimechukuliwa kunatokana na watendaji hao kuhusishwa na tuhuma za
ubadhidilifu ambazo zimebainika kufanyika katika taasisi hiyo. Maeneo
ambayo yamebainika kuwa na ukiukwaji mkubwa ni pamoja na kufanya malipo
kwa kutumia mikataba isiyosainiwa na pande zote, kufanyika malipo
kinyume na taratibu za manunuzi na hata malipo kufanyika kwa fedha
taslim kinyume na taratibu.
Aidha,
eneo la manunuzi ya viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya TBA pia
yameonyesha kuwa na vitendo vya ubadhilifu na ukiukwaji wa taratibu.
Vipo viwanja vilivyobainika kununuliwa nje ya taratibu, baadhi ya
nyaraka kuonyesha ukubwa tofauti na ule uliolipiwa, kununua maeneo
yasiyofaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Serikali, kuongeza bei na
kufanyika kwa malipo kabla ya mikataba kusainiwa.
Hatua
zilizochukuliwa ni muendelezo wa juhudi za Wizara za kuhakikisha kuwa
maeneo yote yanayoashiria kuwa na utendaji ulio nje ya maadili
yanafuatiliwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za
utumishi wa umma.
Aidha,
ili kuboresha ufanisi katika Wakala hivi karibuni waliteuliwa Mameneja
wapya 15 wa TEMESA katika mikoa mbali mbali hapa nchini ikiwa ni pamoja
na kuwahamisha vituo mameneja wengine. Kwa upande mwingine, ajira za
Watendaji katika vituo vyote vya mizani tayari zimetangazwa na kwa sasa
kazi ya kupitia maombi yaliyowasilishwa inakamilishwa ili kuhakikisha
kuwa watendaji wasio waaminifu hawapati nafasi katika maeneo hayo ambayo
yamekuwa yakilalamikiwa kwa vitendo vya ubadhirifu.
Wizara
itaendelea kuchukua hatua za aina hii pale ukiukwaji wa sheria na
taratibu za utumishi wa umma utakapobainika.
Taarifa
hii imetolewa na;
M.S.
Ntemo
MSEMAJI
WA WIZARA YA UJENZI