Dar es
Salaam. Sakata la Mkuu wa Itifaki wa Ikulu, Anthony Itatiro, ambaye
anahusishwa na njama za kutaka kuchota kiasi cha Sh3 bilioni kwa ajili
ya safari hewa ya Rais, limechukua sura mpya baada ya Kamati ya Bunge ya
Mambo ya Nje kutaka kujua hatima ya kigogo huyo jana.
Itatiro na maofisa wanne wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walituhumiwa mwaka jana
kuidhinisha kuchota kiasi hicho cha fedha bila ya kuwapo kwa ziara ya
Rais kwenda nchi yoyote ya kigeni.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Juma Mahadhi
alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa swali na Mwenyekiti wa Kamati ya
Mambo ya Nje ya Bunge, Edward Lowassa.
Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli
aliuliza swali hilo ghafla kwa Mahadhi wakati akitoka nje, baada ya
kumalizika kwa kikao cha kamati yake kilichofanyika kwenye ofisi za
Bunge jijini Dar es Salaam.
Mahadhi, ambaye alilazimika kutoa
ufafanuzi wa swali hilo baada ya kubanwa zaidi na waandishi wa habari,
alisema Rais Kikwete ndiyo mwenye mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya
Itatiro kutokana na ripoti ya uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi wa Ndani wa Wizara hiyo.
Alisema pia kuwa walishauriwa kuwa
maofisa walioshirikiana na Itatiro nao wachukuliwe hatua za kinidhamu
kufuatia njama hizo.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo,
Katibu Mkuu Ombeni Sefue hakupokea simu. Pia hakujibu pindi alipotumiwa
ujumbe mfupi kwa njia ya simu. Naye Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Utumishi, George Yambesi alisema hakuwa tayari
kuzungumzia suala hilo kwani alikuwa likizo.
Mahadhi alisema wakati tukio hilo
linatokea viongozi wakuu wa wizara hiyo walikuwa kwenye majukumu mengine
ya Serikali, jambo ambalo lilisababisha nafasi zao kukaimiwa na
watendaji hao.
“Wale maofisa walitumia mwanya wao wa
kukaimu nafasi ile ndiyo wakasuka mpango huo,” aliongeza Mahadhi.
Alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya
maofisa hao wamechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo ya kuwashusha vyeo
na kuwabadilisha vitengo.
Mahadhi alisema kwamba huwa ni utaratibu
wa kawaida kwa Rais anaposafiri maofisa wa Itifaki na wale wa Wizara ya
Mambo ya Nje kupewa fedha na hazina kwa ajili ya kufanikisha ziara zake.
No comments:
Post a Comment