Msemaji wa klabu ya simba Ezekiel Kamwaga akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana
KIKAO cha
Kamati ya Utendaji ya Simba SC jana, kimefikia uamuzi wa kuitisha
Mkutano Mkuu wa dharula wa klabu hiyo, ambao ajenda yake itakuwa moja
tu, kujadili mwenendo wa timu katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari mchana wa leo, makao makuu ya klabu, Mtaa wa
Msimbazi, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga
amesema kwamba siku na mahali ambako Mkutano huo utafanyika vitatajwa
wakati wowote kuanzia sasa.
Aidha,
Kamwaga alisema kwamba hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Simba SC
aliyejiuzulu na kwamba uongozi upo pamoja. “Hadi sasa hakuna kiongozi
yeyote wa klabu ya Simba aliyejiuzulu. Uongozi upo pamoja na mambo yote
yatajadiliwa kwenye mkutano huo wa dharula,”alisema.
Akiuzungumzia
mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika,
Kamwaga alisema kwamba timu itaondoka Alfajiri ya Ijumaa kwenda Angola
kuwavaa wenyeji wao, Recreativo de Libolo.
Alisema mechi hiyo itafanyika Jumapili mjini Calulo, umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda.
“Kwa mujibu
wa kanuni za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) kama umbali wa mji ambao
inachezwa mechi unakuwa ni zaidi ya kilomita 200, timu mwenyeji
inatakiwa kumsafirisha mgeni kwa ndege, kwa hivyo ni matumaini yetu,
wenyeji wetu watakuwa tayari wametutayarishia ndege, kwa kuwa hatuwezi
kusafiri kwa basi kwa zaidi ya saa nne,”alisema Kamwaga.
Kamwaga
alisema kwamba, Mkuu wa msafara wa timu atakuwa Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans
Poppe, wakati upande wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utawakilishwa
na Mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji pia, Muhsin Balhabou.
Kamwaga
alisema kikosi kamili cha Simba kitakachokwenda Angola kitatajwa
Alhamisi kwa kuwa leo ni mapema sana, kwani wanahofia anaweza kuumia
mchezaji yeyote wakati amekwishatajwa kuwemo kwenye safari.
Simba SC
ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza na Libolo wiki iliyopita
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ili isonge mbele, inatakiwa kushinda
2-0.
Mwaka 1978,
Simba iliwahi kufanya maajabu ikitoka kufungwa 4-0 na Mufulira
Wanderers ya Zambia mjini Dar es Salaam katika michuano hiyo hiyo na
kwenda kushinda 5-0 ugenini, hivyo kusonga mbele.