RAIS Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete, ametengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, huku pia akitengua
kitendawili cha nani mmiliki wa fedha za akaunti ya Escrow na kusema sio
za umma bali ni za IPTL.
Aidha, Serikali kupitia Kamati ya Maadili inaendelea kumfanyia uchunguzi kwani kuna upungufu wa kimaadili umeonekana kutendeka.
Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa
anahutubia taifa kupitia wazee na wakazi wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi
wa Diamond Jubilee, lengo likiwa kuzungumzia mambo mbalimbali ya
kitaifa, yakiwemo yale yaliyokuwa yakisubiri uamuzi wake, kubwa
likitajwa la sakata la Akaunti ya Escrow.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz,
ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali
na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715
221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Baada ya kutoa historia ndefu ya Kampuni ya Kufua Umeme ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL), tangu kuanza kwake hadi
sakata la Escrow, Rais Kikwete alianza kujibu na kutolea maamuzi
maazimio nane ya Bunge, huku lililokuna wengi likiwa la kuwajibisha
viongozi waandamizi, wakiwemo mawaziri katika serikali yake na pia Bodi
ya Wakurugenzi ya Tanesco.
Akizungumzia hilo, alisema Bodi ya Tanesco imeshamaliza muda wake,
hivyo ni kama imeshajifuta, aidha, suala la kutengua uteuzi wa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, amezitaka mamlaka
zinazohusika zianze uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na endapo
zitathibitika, atawajibishwa.
“Nimeagiza mamlaka husika zifanye uchunguzi na iwapo tuhuma dhidi
yake zitabainika hatua stahiki zitachukuliwa, ikiwepo kumwajibisha,”
alisema Rais Kikwete.
Aidha, alisema tayari Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema
ameshajiuzulu ingawa amekuwa akisisitiza kuwa, hakuna kosa alilolifanya
bali amewajibika ili kubeba `msalaba’ wa wengine aliokuwa anawashauri,
hivyo amejiwajibisha huku akiongeza kuwa, kuhusu Profesa Tibaijuka
amezungumza naye na kukubaliana aachie ngazi.
Muhongo awekwa kiporo
Wakati akichukua uamuzi huo dhidi ya Profesa Tibaijuka, Rais Kikwete
alitangaza kumweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, kwani suala lake liko katika hatua za kiuchunguzi.
“Kuhusu Muhongo tumemuweka kiporo, kuna uchunguzi nimeagiza ufanywe
na matokeo yake yanaweza kuja baada ya siku mbili na nitafanya maamuzi
kwa haki,” alisema Rais Kikwete.
Maswi na Muhongo walikuwepo ukumbini wakati Rais anahutubia, ilhali Profesa Tibaijuka hakuwepo.
Tuhuma za Tibaijuka
Akizungumzia tuhuma za Tibaijuka, Rais alisema: “Tumezungumza naye na
Kamati ya Maadili inaendelea kuzungumza naye, na msingi wa mazungumzo
yetu ni fedha alizopewa ni za nini na alisema ni za kuendesha shule, ila
kwa nini hazikuenda moja kwa moja kwenye akaunti ya shule?
Ila akasema masharti ya watoaji (VIP Engineering), ndio yalitaka
hivyo, ila kimsingi kuna upungufu wa kimaadili hapa na sina hakika kama
hawa wanaopitapita kwenye akaunti wanaona nini. Tumekubaliana atupe
nafasi tumteue mwingine.“ alisema Rais Kikwete.
Maazimio mengine ya Bunge aliyoyatolea uamuzi ni la kutaifisha
mitambo ya IPTL na kuipa Tanesco, ambapo alisema; “Ni jambo
linalojadilika na Serikali imelipokea na kulijadili, ila kutaifisha
mitambo wakati huu wa kuwavutia wawekezaji si jambo sahihi na litaleta
picha mbaya kwa wawekezaji. Tulishaacha hayo masuala ya kutaifisha.”
Aidha, alisema Mahakama iliagiza IPTL, kushusha bei ya umeme na
kampuni hiyo ikaagizwa kubadilisha mitambo yake ya kufua umeme kutoka ya
dizeli kuwa ya gesi na kwamba maagizo hayo ni mazuri, kwani umeme
utakuwa ukinunuliwa kwa bei ndogo.
Kuhusu uwazi wa mikataba, alisema serikali itafanya mapitio ya
mikataba, na kuongeza kuna haja ya Serikali na Bunge kukaa pamoja na
kuzungumza jinsi ya kwenda na jambo hilo kwani kuna makampuni yanataka
usiri wa mikataba .
Aidha, akizungumzia azimio la kuwavua vyeo wenyeviti wa Kamati za
Bunge, alisema suala hilo lipo katika mamlaka za Bunge husika. Kuhusu
kuundwa kwa Tume ya Kijaji kuwachunguza majaji waliohusika na sakata la
Escrow, alisema itabidi kuzingatia utaratibu wa kikatiba na sheria.
Alisema suala hili linatakiwa kuanzia kwenye mahakama, badala ya
kuanzia kwa Rais au bungeni, hivyo amemwachia Jaji Mkuu alishughulikie
suala hilo na kwamba anachosubiri ni mapendekezo ya hatua za kuchukua.
“Tume ya Majaji ndio wanapaswa kujadili jambo hili na sio lianzie
kwangu, ila nimemwambia Jaji Mkuu alishughulikie hili na wakiona majaji
hao wamepoteza sifa na wakaleta uamuzi kwangu kwani mimi ndiye ninapewa
majina ya kuteua, nitafanya maamuzi ,” alisisitiza Rais.
Akizungumzia azimio la kutaka mamlaka husika za kifedha na
kiuchunguzi ziitaje Benki ya Stanbic na nyingine zilizohusika katika
sakata la Escrow zitangazwe kuwa taasisi zinazotakatisha fedha alisema
ni pendekezo zuri ila uchunguzi ufanywe.
“Ni jambo zuri na uchunguzi ufanywe,tunavyo vyombo vya uchunguzi vya
ndani watafanya kazi hiyo”, alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete pia
alizungumzia uundwaji wa mamlaka za kushughulikia rushwa kubwa na ndogo,
akisema serikali iandae na kuwasilisha marekebisho ya sheria ya
uundwaji wa vyombo hivyo.
Alisema ni wazo zuri, na serikali imekuwa inaifanyia marekebisho Taasisi ya Kuzuia Rushwa tangu mwaka 2008. Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz,
ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali
na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715
221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Akaunti ya Escrow
Kuhusu nani ni mmiliki wa akaunti ya Escrow na iwapo fedha ni za umma
au hapana, Rais alifafanua kuwa umiliki wa akaunti hiyo ni tofaati na
akaunti nyingine na kwamba akaunti hiyo ilifunguliwa chini ya usimamizi
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambapo ilikuwa ni kuweka fedha za IPTL
kutoka Tanesco.
“Baada ya kuwa na mzozo baina ya Tanesco na IPTL, waliamua kufungua
akaunti ambayo fedha zitakuwa zinahifadhiwa huko wakati mzozo wao
wakiendelea kuutafutia suluhu na akaunti hiyo waliifungua Julai 5,mwaka
2006,” alisema Rais Kikwete.
Na Kwamba fedha zilizokuwa zikiwekwa humo ni za madai ya tozo la
uwekezaji ambalo kampuni ya IPTL iliidai Tanesco hivyo, fedha hizo ni za
IPTL na sio za Umma na kwamba Mamlaka ya Mapato nchini TRA,
ilishapeleka madai ya kodi ya serikali ya ongezeko la thamani kwa IPTL
na wamekubali kulilipa.
“Kwa mantiki hiyo fedha sio za umma ni za IPTL ambaye ndiye mlipwaji
madai yake kutoka Tanesco,” alisema Rais Kikwete na kuongeza tangu
akaunti hiyo ifunguliwe miaka saba sasa kwa bahati mbaya Tanesco
haikufanikiwa kufikia suluhu na IPTL hadi kampuni hiyo ikapewa malipo
yake.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete, imefuta hisia kwamba fedha za IPTL zilizoibua mjadala mkali bungeni zilikuwa za umma.
Ndani ya Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliomalizika Novemba 28 mwaka
huu, wabunge walichachamaa na kutaka serikali iwawajibishe wote
waliohusika na kutafuna fedha za IPTL zaidi ya Sh bilioni 300, huku
ikisisitizwa kuwa ni za umma, jambo ambalo Rais Kikwete amethibitisha
kuwa ulikuwa upotoshaji.
Wakati Rais Kikwete akizungumzia suala hilo, Profesa Muhongo alikuwa
ni miongoni mwa mawaziri waliohudhuria akiwamo pia Maswi. Wengine ni
pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba na wengineo. Hata hivyo, Profesa Tibaijuka hakuhudhuria mkutano
huo.
Kauli ya Zitto
Akizungumzia uamuzi wa Rais Kikwete, Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto
alisema: “Nimemsikiliza Mheshimiwa Rais. Ninachoweza kusema ni kwamba
maazimio yale hayakuwa ya Zitto Kabwe, PAC, CAG au PCCB. Yalikuwa ni
maamuzi ya Bunge zima. Bunge la vyama vyote kikiwamo chama cha Rais
Kikwete yaani CCM.
“Sisi kama Bunge tulitoa maazimio yale kwa maridhiano, uzalendo na
bila kutaka kumuonea mtu yeyote. Suala hili sasa naliacha kwa wananchi.
Bunge limefanya kazi yake na Serikali ambayo ndiyo tulikuwa tunasubiri
maamuzi yake imeamua hivyo. Wananchi wataamua wenyewe”.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz,
ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali
na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715
221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Na Habari Leo
No comments:
Post a Comment