Mkurugenzi Mstaafu waTaasisi ya Utafiti ya Twaweza, Rakesh Rajan (kulia)
akiwaelezea jambo Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri ya Raia Mwema, Jenerali
Ulimwengu (kushoto) na Mkurugenzi wa Compass Communication Limited,
Maria Sarungi katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa kabla ya taasisi hiyo
kutangaza matoke ya utafiti wao kuhusu Tanzania Kuelekea 2015, jijini
Dar es Salaam juzi.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya
Twaweza kuhusu maoni na matakwa ya wananchi juu ya uongozi wa kisiasa
nchini, umeibua madai mapya ambayo yanauhusisha na jitihada za
kukisaidia chama tawala CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Dar es Salaam juzi,
inaonyesha kuwa kama Uchaguzi Mkuu ungefanyika sasa, Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa angeshinda urais kwa asilimia 13, akifuatiwa na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa asilimia 12, huku Katibu Mkuu wa Chadema
Dk Willibrod Slaa akiibuka na asilimia kumi na moja.
Mbali na wanasiasa hao, wengine waliotajwa katika
ripoti hiyo na asilimia zao kwenye mabano ni Profesa Ibrahim Lipumba
(6%), Dk John Magufuli (3%), Freeman Mbowe (3%), Samuel Sitta (4%),
Bernard Membe (5%) na Zitto Kabwe (1%). Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa iwapo vyama vyote vya
upinzani vitaungana na kumchagua mgombea mmoja wa urais, Dk Slaa
angeongoza kwa asilimia 41, akifuatiwa na Profesa Lipumba (14%), Mbowe
(11%) na Zitto Kabwe (6%). Wengine ni Tundu Lissu, Maalim Seif Sharif
Hamad, James Mbatia na Augustine Mrema ambao kila mmoja aliambulia
asilimia moja.
Dk Slaa
Akizungumzia utafiti huo jana, Dk Slaa alisema
chama chake kinautilia shaka kwani licha ya kuonyesha kwamba umefanywa
na taasisi ya Twaweza, taarifa alizonazo zinaeleza kuwa matokeo yake
yameandaliwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson
Bana.
Dk Slaa alisema Dk Bana anafahamika kuwa na
uhusiano na CCM na kwamba pia anafanya kazi na taasisi nyingine ya
utafiti ya Redet jambo linaloonyesha kuwa utafiti huo umeandaliwa kwa
manufaa ya CCM.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti jana, madai hayo
yalikanushwa na Mkurugenzi wa Twaweza anayemaliza muda wake, Rakesh
Rajani na Dk Bana.
Dk Slaa alisema kuwa amepata taarifa alizoziita za
kutisha kuwa mmoja wa viongozi nchini (hakumtaja jina) alituma
baruapepe kwenda kwa kiongozi mwingine akimwambia kuwa bosi wake
atafurahi kwa kuwa kazi aliyowatuma wameimaliza.
“Taarifa hii imetushtua na tunaendelea kuifanyia
kazi,” alisema Dk Slaa. Alisema alisoma ripoti ya Twaweza siku tano
kabla ya uzinduzi na kwamba alibaini kuwa zaidi ya asilimia 50 ya
wananchi waliohojiwa walikuwa ni wazee.
“Tunataka kujua jambo hili lilifanyika kwa makusudi au lilikuwa na maana gani?”
Katibu Mkuu huyo aliikosoa ripoti hiyo kuwa
iliwezaje kutabiri mambo kabla hayajatokea kwa kueleza kuwa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) ungeungana na kumsimamisha mgombea mmoja wa
urais.
“Ukitazama taarifa imetolewa lini na maswali yaliulizwa lini
utashangaa. Kwa nini unaweka mkokoteni mbele ya punda?” alihoji Dk Slaa.
Hata hivyo Twaweza katika ripoti yake inaeleza bayana kwamba iliuliza
swali kuhusu mgombea mmoja wa upinzani ikiwa vyama hivyo vitaungana.
“Wakati tunafanya utafiti huu vyama vinavyounda
Ukawa vilikuwa havijasaini makubaliano ya kuwa na mgombea mmoja lakini
kwa sababu tulishaona dalili na kusikia tetesi, basi tuliamua kuuliza
swali hili. Kwa hiyo kwa kuwa sasa tayari vyama hivyo vimeshasaini
makubaliano, utafiti mwingine unaweza kuwa na matokeo tofauti kabisa,”
alisema Mwasilishaji wa Utafiti huo, Elvis Mushi juzi.
Rakesh atoa ufafanuzi
Akizungumzia tuhuma za kumtumia Dk Bana kufanya
utafiti huo, Rakesh alisema siyo za ukweli kwa kuwa matokeo yanaonyesha
kuwa walioshinda ni wananchi asilimia 33 ambao hawajaamua kumpigia kura
mgombea wa chama chochote.
“Siwezi kusema kama Dk Bana anatumiwa na CCM,
lakini ninachojua ni kuwa tulimwalika kushiriki kama mchangia mada kama
watu wengine walivyofanya,” alisema.
Kuhusu kundi la wananchi ambao hawajaamua mtu wa
kumpigia kura, Rakesh alisema ni vyema hata kama mtu angesema CCM haifai
kutokana na matokeo hayo kwa kuwa wagombea wote wamepata chini ya
asilimia 15.
Alisema watu wanaoisoma ripoti hiyo kwa kuangalia
majina ya watu maarufu wanafanya makosa kwa sababu mwanafunzi hawezi
kushangilia kwa kupata maksi ndogo.
“Hivi wewe ukipata mtihani mmoja asilimia 13 na
mwingine 33, upi utakuwa umefaulu?” alimhoji mwandishi na kuongeza:
“Asilimia 33 ndiyo unakuwa umefaulu.”
Alisema Twaweza imefanya tafiti za Sauti za
Wananchi mara 24 na kwamba wamekuwa wakifanya kwa uadilifu wa hali ya
juu. Alifafanua kuwa Watanzania wanafurahi pale matokeo ya utafiti
yanapokuwa mazuri kwao, lakini hukasirika yanapokuwa kinyume.
Dk Bana ajitetea
Kadhalika, Dk Bana alikanusha tuhuma zilizotolewa
na Dk Slaa dhidi yake akisema hajawahi kuwa na uhusiano na Twaweza huku
akidai kuwa hata yeye mwenyewe anatamani CCM itoke madarakani miaka
mitano tu, ili wananchi wapate uongozi tofauti.
“Kwa kweli ningekuwa na simu ya Dk Slaa
ningempigia. Chadema na Ukawa wakijipanga wanaweza kuchukua nchi maana
wana ushawishi mkubwa kwenye vyombo vya habari na makundi ya jamii.
“Kosa walilolifanya ni kumtimua Zitto Kabwe, ni kama vile
Barcelona bila (Lionel) Messi. CCM sasa hivi imechokwa wananchi wanataka
kuona uongozi tofauti,” alisema Dk Bana.
Alisema kitendo cha Chadema kumhusisha na CCM
kitakwamisha mpango wake wa kujiunga na chama hicho ili agombee ubunge
katika Jimbo la Bukoba Vijijini... “Ingawa familia yangu haipendi
niingie kwenye siasa, bado naendelea kufikiri, lakini kwa mambo haya
(Chadema) watanikubali kweli?” alihoji. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment