Hii ni moja ya picha mbalimbali za wajawazito kama inavyonekani siyo ya mwalimu muhusika kwa tukio hilo.
WAKATI ikiwa imezoeleka kuwa baadhi ya walimu wa kiume huwarubuni
wanafunzi wao wa kike na hata kuwaharibia kabisa ndoto zao za kielimu
kutokana na kuwapa ujauzito, hali imekuwa tofauti mkoani Rukwa ambako
mwanafunzi wa Kidato cha Pili anadaiwa kumzalisha mwalimu wake.
Mwanafunzi huyo aliyemzalisha mwalimu wake ana umri wa miaka 17, wakati
mwalimu huyo anayefundisha katika Shule ya Sekondari ya Umma ya Nkasi,
iliyopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa, ana umri wa
miaka 25.
Tukio hilo linalotajwa kuwa la kwanza kutokea wilayani hapa, limekuwa gumzo kubwa kwa wakazi wa Nkasi na wilaya jirani.
Hata hivyo, kwa wanafunzi, wamekuwa wakimpongeza mwenzao kwa kujaliwa
kupata mtoto katika umri wake huo mdogo, huku mzazi mwenzake akiwa na
uhakika wa maisha kutokana na kuwa ni mtumishi serikalini. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Imeelezwa kuwa licha ya tukio hilo, mwalimu huyo aliyezaa na mwanafunzi
wake bado anaendelea na masomo shuleni hapo, huku `mzazi’ huyo wa kiume
akifundishwa na mzazi mwenzake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Namanyere hivi karibuni,
Mkuu wa Shule ya Sekondari Nkasi mjini Namanyere ambayo ni ya
mchanganyiko ya umma, Amiamie Nanga alisema mwalimu huyo alianza kazi
shuleni hapo ikiwa ni mara yake ya kwanza kufundisha baada ya kuhitimu
mafunzo ya ualimu chuoni.
“Yameshatokea, lakini haileti picha nzuri sana, lakini mimi nina uzoefu
mkubwa na wakazi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika, kwao si ajabu kuwa na
uhusiano na watu waliowazidi umri, iwe kwa mtoto wa kike au wa kiume,
wote ni sawa tu…
“Lakini katika kisa hiki, inaonesha walimu sasa wanapoteza haiba ya
ualimu. Hii kazi ina miiko na maadili yake …kwa mwalimu huyu hii ni
ajira yake ya kwanza, nikimaanisha ni kituo chake cha kwanza cha kazi
tangu ahitimu masomo yake…” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob
Mwaruanda alisema hakuna kosa kwa mwalimu huyo wa kike kwa kuwa tayari
ni mtu mzima.
“Isitoshe katika kisa hiki ni nadra kumpata mlalamikaji … Mwalimu
mwenyewe huyu wa kike hawezi kuwa tayari kujidhalilisha kuwa amebakwa,
yalikuwa maamuzi yake.”
Aliongeza kuwa, kwa mwalimu huyo kupata ujauzito wa mwanafunzi wake
hakuwezi kuathiri ajira yake, tofauti na mwalimu wa kiume akimpatia
ujauzito mwanafunzi wake wa kike ambaye huathirika kwa kukatisha masomo.
Jitihada za kumpata mwalimu huyo wa kike na mwanafunzi huyo zimegonga
mwamba baada ya watu wao wa karibu kumweleza mwandishi kuwa hawako
tayari kuuzungumzia mkasa huo.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliohojiwa na mwandishi wa habari
hizi kwa masharti ya kutoandikwa majina yao kwa hofu ya kuchukuliwa
hatua za kinidhamu shuleni hapo, pamoja na kukiri kutambua uhusiano
baina ya mwanafunzi mwenzao na mwalimu wao, lakini walisema hivi sasa
mwalimu huyo amesitisha uhusiano na mwenzao na kuanzisha uhusiano mpya
na mwalimu mwenzao.
Walisema pamoja na mambo mengine ni kama mwanafunzi mwenzao ameathirika
kisaikolojia baada ya ‘kupinduliwa’ na mwalimu wake wa kiume ambaye kwa
sasa ndiye baba mlezi wa mtoto.
“Huyu mwalimu wa kike sisi sasa tunamwita shemeji yetu alikuwa na
uhusiano wa kimapenzi na mwenzetu… penzi lao lilikolea hadi sasa ameweza
kumzalia mtoto huyo…, lakini kwa sasa inavyoelezwa ni kwamba penzi
limehamia kwa mwalimu mwenzake,“ alisema mmoja wao.
Baadhi ya watu wa karibu na mwanafunzi huyo wanakiri kuwa mwanafunzi
huyo hana uwezo wa kifedha kumudu kumpatia malezi stahiki mtoto wake
huyo, hivyo hata mzazi mwenzake alipoanza uhusiano na mwalimu mwenzake
hakuwa na jinsi, bali kukubaliana na matokeo.
“Usiniandike jina, sisi tunashauri mwalimu huyo wa kike na mpenzi wake
huyo wa kiume ambaye ni mwalimu mwenzake wahamishiwe shule nyingine kwa
sababu kama kioo katika jamii wameteleza kwa kiasi kikubwa na
watashindwa kuwajenga na kuwalea wanafunzi wao kimaadili.
“Isitoshe tunajiuliza sheria hapa inasemaje maana kama angekuwa ni
mwalimu wa kiume amempatia mwanafunzi wake wa kike ujauzito
angeshitakiwa na kufikishwa mahakamani na pengine kuhukumiwa kifungo
kisichopungua miaka 30 jela, sasa kwa hili sheria inasemaje?”Alihoji.
Baadhi ya wazazi mkoani hapo waliohojiwa na mwandishi kwa nyakati
tofauti wameelezea kushangazwa na tukio hilo, na hasa kwa jinsi mwalimu
alivyoshindwa kujizuia `kujiachia’ kimapenzi kwa mwanafunzi wake.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment