Mkurugenzi wa
Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare leo anatarajiwa kuchuana
upya na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wakati Mahakama ya Rufani
itakaposikiliza maombi ya marejeo ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyomfutia
mashtaka ya ugaidi.
Maombi hayo Namba 5 ya mwaka 2014, yalifunguliwa
na DPP akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kumfutia
Lwakatare mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake,
Joseph Ludovick.
Katika maombi hayo, DPP anaiomba Mahakama ya
Rufani iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi wa
Mahakama Kuu kuwafutia washtakiwa hao mashtaka ya ugaidi na kisha ifute
uamuzi huo wa Mahakama Kuu na amri zote ilizozitoa.
Pamoja na mambo mengine, DPP anadai kuwa haikuwa
sahihi Mahakama Kuu kuamua kuwa mashtaka hayo hayakuwa halali, kwani
hapakuwa na taarifa zilizowasilishwa dhidi ya washtakiwa ambazo Mahakama
Kuu ingezizingatia katika kuamua uhalali wake. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Maombi hayo yamepangwa kusikilizwa leo na jopo la
majaji watatu linaoongozwa na Jaji Nathalia Kimaro, akishirikiana na
William Mandia na Profesa Ibrahim Juma.
Lwakatare na Ludovick walikuwa wakikabiliwa na
mashtaka manne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, matatu kati yake
yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai.
Mashtaka hayo ya ugaidi yalikuwa ni kupanga
kumteka aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky
na kisha kumdhuru kwa sumu, kushiriki mkutano wa vitendo vya ugaidi
(kwa washtakiwa wote) na kuhamasisha vitendo vya ugaidi lililokuwa
likimkabili Lwakatare pekee.
Shtaka jingine la jinai lilikuwa ni kula njama kutenda makosa, ambalo lilikuwa likiwakabili wote kwa pamoja.
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu Jaji Lawrence Kaduri
wa Mahakama Kuu aliwafutia mashtaka ya ugaidi, baada ya mawakili wa
Lwakatare kufungua maombi wakipinga uamuzi wa DPP wa kuwafutia mashtaka
katika kesi ya awali na kuwakamata upya na kuwafungulia mashtaka
hayohayo.
Katika uamuzi wake, Jaji Kaduri alikubaliana na
hoja za mawakili wa Lwakatare kuwa mashtaka hayo hayana maelezo ya
kutosha kuonyesha kuwa ni ya ugaidi.
Jaji Kaduri alisema kuwa mashtaka hayo yalipaswa
yawe na maelezo yanayoonyesha uhalisia wa ugaidi na kwamba katika
mashtaka hayo kuna makosa kwa kuwa hapakuwa na maelezo ya wazi ya asili
ya ugaidi.
Hata hivyo, Jaji Kaduri alikubaliana na hoja za
Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza kuwa uamuzi wa DPP kufuta kesi
ya kwanza na kuwakamata washtakiwa na kuwafungulia tena kesi yenye
mashtaka hayohayo ulikuwa sahihi.
Lwakatare
na Ludovick walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Machi 18, 2013 na kusomewa mashtaka hayo katika kesi namba 37 ya
mwaka 2013.
Hata hivyo, Machi 20, DPP aliwafutia mashtaka
hayo, kutokana na makosa yaliyofanywa na Mahakama ya Kisutu kuwataka
washtakiwa wajibu mashtaka hayo ambayo yanasikilizwa na Mahakama Kuu,
lakini muda mfupi baadaye walikamatwa na kufunguliwa tena mashtaka hayo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment