Kamati Kuu (CC) ya
Halmashauri Kuu ya CCM inakutana leo mchana mjini Dodoma chini ya
mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete huku ikitarajiwa kufanya uamuzi
mgumu wa mchakato wa Katiba.
Kikao hicho kinaketi mara ya pili katika muda
mfupi, baada ya hivi karibuni kukaa jijini Dar es Salaam na kueleza
kuridhishwa na mchakato huo.
Hata hivyo, safari hii kikao hicho kinaketi kukiwa
na maswali lukuki ambayo hayajapata majibu: Je, Bunge la Katiba
liendelee au livunjwe? Je, lisitishwe kwa muda kupisha maridhiano au la?
Je, kuna umuhimu wa maridhiano? Kuna ulazima wa kuwapo Ukawa bungeni?
Akizungumzia kikao hicho, mtaalamu wa sayansi ya
siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander
Makulilo alisema jambo kubwa litakalojadiliwa katika kikao hicho ni
kauli tofauti zilizotolewa na wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba
Mpya. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba
ameshauri yafanyike maridhiano kwanza na wapo wanaCCM waliomuunga mkono.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema naye ameonyesha
wasiwasi wake, Ukawa na Jukwaa la Katiba Tanzania nao wamesema yao.
Nadhani kuna jambo CCM wameliona na wanataka kuliweka sawa,” alisema Dk
Makulilo.
Aliongeza, “Kujua nini wataamua ni ngumu lakini kutokana na hali ilivyo kwa sasa ni wazi kuwa wanakutana kuona nini kifanyike.”
Kwa upande wake Bashiru Ali alisema, “Tangu mwanzo
mchakato wa Katiba haukuwa katika ilani ya CCM, sasa unaweza kujiuliza
wanakwenda kujadili nini wakati hata katika mikakati yao ya miaka 10 na
20 ijayo hakuna mpango wa kuandika Katiba.”
Habari zilizozagaa mjini Dodoma zinadai kikao
hicho pia kinaweza kupendekeza kuwashughulikia wanachama wake waliotoa
kauli zinazopingana na msimamo wa chama hicho.
Miongoni mwa waliotoa kauli zinazopingana na chama
hicho ni Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba kutokana na
matamshi yake ya kuhoji uhalali wa vikao vya Bunge la Katiba kuendelea
bila uhakika wa akidi.
Mbali na Mwigulu pia wabunge kadhaa wa CCM
akiwamo, Esther Bulaya (Viti Maalumu), Kangi Lugora (Mwibara), Deo
Filikunjombe (Ludewa), Ridhiwani Kikwete (Chalinze) nao wamekaririwa kwa
nyakati tofauti wakitoa misimamo inayokinzana na chama chao kuhusu
uhalali wa Bunge la Katiba kuendelea bila kuwapo maridhiano na Ukawa.
Hata hivyo, habari nyingine zinasema iwapo kuna
mpango huo, Mwigulu anaweza kuondolewa kutokana na utaratibu wa chama
hicho kuwaondoa kwenye sekretarieti wajumbe wake wanaoteuliwa kushika
nyadhifa serikalini.
Chanzo chetu kinasema ikiwa hilo litatokea kwa
sababu ya Mwigulu kuteuliwa Naibu Waziri wa Fedha, basi mpango huo
hautamwacha nyuma Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, Dk AshaRose Migiro
ambaye pia hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza
na gazeti hili jana, alikanusha kuwapo kwa mpango wa kumwondoa Nchemba
katika nafasi yake na kwamba kikatiba kikao chenye uwezo huo ni
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
“Hizo taarifa ni za uongo kabisa, kikao kweli
kitakutana kesho (leo) saa 8:00 mchana chini ya Mwenyekiti Rais Kikwete
na ajenda ni moja tu, ambayo ni mchakato wa Katiba. Kikao maalumu huwa
na ajenda moja maalumu, hakuna mengineyo wala nini,” alisema Nnauye.
Alisema CC itapokea taarifa kuhusu mchakato wa
Katiba unavyokwenda itakayotolewa na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro na baadaye kujadiliwa na wajumbe.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana
zinasema hatua dhidi ya kiongozi huyo wa juu katika chama zinatokana na
kile kinachoelezwa kuwa ni “kuwaudhi makada wa CCM” kutokana na kauli
yake hiyo. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Nchemba jana alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema
kupitia ujumbe mfupi wa maandishi, “Sina taarifa za kung’olewa,
nimealikwa kwenye kikao kama NKM (Naibu Katibu Mkuu wa CCM).”
Hata hivyo, ikiwa CCM itafanya uamuzi wa kumwondoa
Nchemba, huenda ukapokewa kwa hisia tofauti na umma wa Watanzania
ikizingatiwa kwamba pamoja na kutoa kauli zinazokinzana na msimamo wa
chama chake, amekuwa akiungwa mkono na wananchi wa kada mbalimbali.
CC ya CCM ambayo hivi karibuni ilibariki Bunge la
Katiba kuendelea hadi lifike mwisho, inakutana leo kwa dharura wakati
mchakato wa Katiba ukidaiwa kutokuwa na uhalali wa kisiasa kutokana na
kususiwa na idadi kubwa ya wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wanachama
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kutokana na kutokuwapo Ukawa ndani ya Bunge, kuna
hofu kwamba Bunge linaloendelea na vikao vyake Dodoma litakosa theluthi
mbili ya kura kutoka Zanzibar, hivyo kutopatikana Katiba Mpya.
Kutokana na hali hiyo, Mwigulu amekaririwa mara
kadhaa akisema hakukuwa na haja ya Bunge hilo kuendelea na vikao bila
kuwa na uhakika wa kutimiza akidi, vinginevyo itakuwa ni matumizi mabaya
ya fedha za umma, na wananchi hawatawaelewa.
Kutokana na mazingira hayo, vyanzo vya habari
vinasema CCM lazima ifanye uamuzi mgumu wa ama kuziba masikio isisikie
kelele za makundi yanayotaka Bunge lisitishwe hivyo iamue liendelee, au
igeuke jiwe kwa kulisitisha na kukiuka uamuzi wake wa awali.
Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa kwamba
viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakifanya vikao vya siri na wale wa
vyama vya upinzani kwa lengo la kufanyia marekebisho Katiba ya sasa ili
kutengeneza mazingira mazuri ya uchaguzi mkuu mwakani iwapo Katiba mpya
itakwama.
Miongoni mwa maeneo ambayo vyama hivyo
viliyaainisha katika vikao vyake vya siri ni pamoja na kuwapo kwa Tume
Huru ya Uchaguzi, matokeo ya kura za Rais kuhojiwa mahakamani na mgombea
binafsi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment