Mgonjwa wa saratani ya titi
aliyepewa dawa feki za mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
(ORCI) amejikuta katika wakati mgumu baada ya wahudumu wa hospitali hiyo
ya Serikali kumtelekeza alipokwenda kupata tiba.
Mgonjwa huyo, Pendo Shoo ambaye anahofu kwamba
saratani imempata katika titi lake la pili, anasema hatakwenda tena
katika hospitali hiyo na badala yake ameamua kusaka tiba kwa waganga wa
tiba asilia.
Hivi karibuni gazeti hili lilichapisha habari
kuhusu mtumishi wa OCRI, Almasi Matola alivyomtibu Pendo kwa dawa feki
baada ya kumtoza kiasi cha Sh1.34 milioni kinyume na taratibu za tiba
katika hospitali hiyo.
Almasi akizungumza na gazeti hili wiki mbili
zilizopita, alikiri kuwekewa fedha katika akaunti yake ambazo ni zaidi
ya Sh300,000, lakini akakanusha kwamba fedha hizo ni kama ujira wa kumpa
mgonjwa huyo dawa.
Kwa mujibu wa taratibu za OCRI, wagonjwa
wanaokwenda hospitali hapo kwa rufaa kutoka hospitali nyingine hawapaswi
kutozwa fedha zozote kwa ajili ya matibabu. Pendo alipata rufaa kutoka
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Novemba mwaka jana.
Alibaini kuwa alipewa dawa feki baada ya
kutokupata nafuu yoyote wiki kadhaa tangu alipoanza kupewa tiba na baada
ya kuripoti tukio hilo kwa madaktari walimwanzishia upya tiba husika. Wiki moja tu baada ya kuchapishwa habari hizo,
mgonjwa huyo alifika OCRI kuendelea na matibabu lakini alijikuta katika
mazingira magumu kiasi cha kuondoka bila kupewa huduma. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Alisema Jumanne, Mei 20 mwaka huu, alikwenda OCRI
kufuata majibu ya damu aliyokwishapeleka ili kujua iwapo saratani
imesambaa katika titi lingine... “Niliamua kurudi hospitali nikapime
tena. Nilipofika kitengo cha kutoa damu nilitoa kwa ajili ya vipimo,
lakini nilipokwenda tena kuchukua majibu walidai damu yangu imepotea.
Kwa hiyo nililazimika kuanza upya, nilitoa damu tena na vipimo vyote
vikawa tayari kama X-ray, Ultra sound na nikavipeleka kwa daktari.”
Alisema alipatwa na hofu zaidi pale alipokwenda
kwa daktari wake Dk Dominista Kombe ambaye alipaswa kumpa matokeo ya
vipimo, lakini alishangaa pale daktari huyo alipomjibu kwa kusema:
“Majibu yako utayajua hukohuko,” akimaanisha kwenye chumba cha tiba ya
mionzi.
Chumba cha tiba
Alisema alipofika chumba cha tiba ya mionzi
muuguzi aliyekuwapo alimwambia asubiri kwenye foleni hadi atakapoitwa
jina lakini alikaa zaidi ya saa nzima bila faili lake kuitwa. Alisema baadaye muuguzi alirudi na kumwambia aende
nyumbani kwa sababu wagonjwa ni wengi. Lakini wagonjwa wengine
waliokuwa kwenye foleni hawakupewa maelekezo hayo.
“Kwa mazingira niliyoyaona, pale hospitali
wameshaanza kuninyanyapaa kiasi kwamba naogopa. Kwa mfano, daktari
niliyemtegemea anihudumie kwa upendo, juzi alinihudumia bila hata
kuniangalia usoni, nilitegemea anipe majibu na ushauri hakufanya hivyo
na kuniambia niende chumba cha chemo,” alisema Pendo.
Jana gazeti hili lilimtafuta Dk Kombe kupitia simu
yake ya kiganjani na baada ya kupokea kisha mwandishi kujitambulisha
mazungumzo yalikuwa hivi:
Mwandishi: Haloo Dk Kombe…
Dk Kombe: Haloo, nani wewe?
Mwandishi: Ni mwandishi wa Gazeti la Mwanachi
Dk Kombe: Wale mliotuandika kwenye gazeti juzi?
Mwandishi: Ndiyo... (Baada ya majibu hayo, daktari
huyo alikata simu na kila alipopigiwa hakupokea na baadaye simu yake
ilizimwa kabisa).
Mkurugenzi wa Tiba wa OCRI, Dk Diwani Msemo
alisema iwapo kuna wafanyakazi wanaonyanyapaa wagonjwa kama alivyodai
Pendo, ni lazima uongozi wa hospitali ungechukua hatua.
“Huyo mgonjwa alikwenda kulalamika kwa uongozi wa
hospitali? Kuna ofisi ya huduma za jamii, kuna Ofisi ya Mkurugenzi je,
alikwenda?” alihoji Dk Msemo.
Alisema uongozi wa hospitali ungekuwa umegundua
kama kuna unyanyapaa wa aina yoyote, basi waliofanya hivyo wangehojiwa
na kuchukuliwa hatua na kwamba hatua hizo hutegemea kama mgonjwa
ameripoti tatizo husika.
Kauli ya Dk Nsemo inatofautiana na ile iliyotolewa
wiki mbili zilizopita na Mkurugenzi wa OCRI, Dk Twalib Ngoma ambaye
alisema mgonjwa aliyefanyiwa vitendo hivyo anapaswa kwenda kushtaki
kwenye vyombo vya sheria.
“Anakuja kwako kulalamika wewe umsaidie nini,
anatakiwa kwenda katika vyombo vya sheria ili apewe haki yake, wewe
utamsaidiaje?” alihoji Dk Ngoma.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja alisema mgonjwa huyo kama anaona ameonewa anapaswa kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali hiyo... “Amekwenda kushtaki kwa uongozi? Unajua Ocean Road ni taasisi inayojitegemea, anatakiwa akashtaki huko…” Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Na Florence Majani, Mwananchi
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja alisema mgonjwa huyo kama anaona ameonewa anapaswa kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali hiyo... “Amekwenda kushtaki kwa uongozi? Unajua Ocean Road ni taasisi inayojitegemea, anatakiwa akashtaki huko…” Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Na Florence Majani, Mwananchi
No comments:
Post a Comment