HATUTAKI, na tena hatutaki hata kusikia. Na ikiwezekana msirudi tena. Ndivyo ambavyo mapovu yamewatoka mdomoni watu wa Manchester United baada ya PSG kurudi mezani juzi Jumapili na ofa ya kumtaka kinda wao mahiri, Adnan Januzaj.
PSG wamekuwa wakitokwa udenda kwa
kinda huyo mwenye asili ya Albania aliyezaliwa Ubelgiji miaka 18
iliyopita na hawajali kama aliingia mkataba mpya wa kuichezea Man United
mwishoni mwa msimu uliopita.
Hata hivyo, kocha David Moyes amekataa
ofa hiyo ya PSG inayodhaniwa kuanzia Pauni 25 milioni na kuendelea huku
wakisisitiza kwamba hawana mpango hata wa kukaa chini na kuzungumza na
matajiri hao wa mafuta kutoka Paris.
Man United imempatia mkataba mrefu wa
miaka mitano Januzaj Oktoba mwaka jana baada ya kugundulika kuwa huenda
mchezaji huyo angekuwa huru na kuondoka Mei mwaka huu mara baada ya
msimu kumalizika.
Kabla na baada ya kusaini mkataba huo,
Januzaj ameibuka kuwa miongoni mwa wachezaji wachache mahiri katika
kikosi cha Man United ambacho msimu huu kimekuwa kikisuasua ndani ya
uwanja.
Kwa mujibu wa gazeti la Guardian la
Uingereza, Januzaj angeingiza kiasi kikubwa cha pesa kama angeamua
kukubali kwenda PSG, lakini mwenyewe ameamua kubaki Man United licha ya
timu hiyo kuwa katika hatari ya kukosa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya
msimu ujao.
Katika mkataba wake wa awali nyota
huyo alikuwa akiingiza kiasi cha Pauni 1,000 tu kwa wiki kutokana na
kuwa kinda mwanafunzi, lakini mkataba wake wa sasa unamwingizia kiasi
cha Pauni 30,000 kwa wiki.Akiwa na PSG angeweza kuingiza kiasi cha zaidi ya Pauni 80,000 kwa wiki, lakini staa huyo ameamua kubaki Man United na kuendelea kujifunza zaidi wakati huu kocha Moyes akimwamini na kumpanga mara nyingi zaidi katika safu ya ushambuliaji.
Wakati huohuo pia, PSG pia imekataliwa
katika ofa yao ya Pauni 14 milioni kwa ajili ya kumchukua kiungo mahiri
wa Newcastle United, Yohan Cabaye ambaye amekuwa akisakwa kwa muda
mrefu na kocha Laurent Blanc.
Newcastle inaamini kuwa staa huyo
Mfaransa ana thamani ya Pauni 25 milioni na inadaiwa kuwa hata Man
United wameanza kumtolea macho Cabaye. Chanzo: mwanaspoti
No comments:
Post a Comment