Polisi
nchini Kenya wamewahoji maafisa wakuu watendaji wa kampuni za huduma za
simu za rununu kuhusu usajili wa kadi za simu za mkononi zinazotumia
huduma za kampuni hizo.
Hatua ya polisi imefuatia ripoti kuwa
simu zenye kadi ambazo hazikuwa zimesajiliwa zilitumiwa na magaidi
walioshambulia jumba la Westgate mjini Nairobi wiki mbili zilizopia.
Wanne hao walitishiwa kukamatwa mnamo
siku ya Jumatatu baada ya maafisa wa serikali kuwatuhumu kwa kuuza kadi
za simu ambazo hazijsajiliwa.
Hata hivyo walikana tuhuma hizo.
Mnamo mwaka 2010, serikali ya Kenya
ilieleza kuwa sharti mmiliki wa simu kusajili kadi yake ya simu ya
mkononi katika hatua ya serikali kuzuia visa vya uhalifu wa kutumia simu
za mkononi. Hata hivyo sheria ilianza kutekelezwa mwaka jana.
Takriban watu 67 waliuawa kwenye
mashambulizi hayo na wengine wengi kujeruhiwa kwenye mashambulizi
yaliyofanywa na kundi la kigaidi la al-Shabab .
Katika taarifa yao ya pamoja, maafisa
hao wakuu wa kampuni za huduma za simu,Safaricom, Bharti Airtel, Orange
Kenya na Yu Essar – walisema kuwa walitoa taarifa kwa polisi asubuhi ya
leo.
Walikanusha madai ya kuwepo simu ambazo hazijasajiliwa na kusema kuwa wanafuata masharti yakimataifa kuhusu usalama.
Lakini kwenye mahojiano na BBC mkuu wa
tume ya mawasiliano ya Kenya, Francis Wangusi alisema kuwa polisi wana
ushahidi ulio kinyume na madai ya maafisa hao.
Kwamba watu wangali wanatumia kadi za simu ambazo hazijasajiliwa.
Wakenya milioni 29 wamesajili kadi zao za simu wakati wengine milioni 1.6 wanatumia kadi zisizosajiliwa.
Haya yanajiri baada ya taarifa kusema
kuwa polisi wanajaribu kutafuta nambari za simu zilizotumiwa na watu
waliohusika na shambulizi la kigaidi dhidi ya Westgate na kusababisha
vifo vya watu 67 huku mamia zaidi wakijeruhiwa.
Mnamo Jumatatu wakuu wa kampuni za
huduma za simu na mawakala wao walionywa kuwa huenda wakakamatwa kwa
makosa ya uhalifu na kukosa kusajili kadi za simu za wateja wao.
Waziri wa mawasiliano Fred Matiang'i
alisema kuwa polisi wanafanya msako kote nchini kuwatafuta wale
wanaokiuka sheria inayoshurutisha usajili wa kadi za simu iwe ni wakuu
wa kampuni za simu au mawakala wao.
No comments:
Post a Comment