Kumekuwa na kelele za waumini nchini Ujerumani wakishinikiza askofu huyo afukuzwe kwa kukiuka taratibu.
Vatican City. Makao Makuu ya Kanisa
Katoliki Duniani (Vatican) yamemsimamisha kazi Askofu wa Jimbo la
Limburg, Ujerumani Franz-Peter Tebartz-van Elst anayekabiliwa na kashfa
ya matumizi mabaya ya fedha kwa shughuli za kifahari.
Vatican ilieleza jana kuwa uamuzi huo
umechukuliwa baada ya kuridhika kuwa Askofu van Elst amekiuka maadili
yaliyowekwa na Papa Francis kwa viongozi walioko chini yake akiwataka
waishi maisha ya uchaji, umaskini.
Hadi sasa, kumekuwa na kelele nyingi miongoni mwa waumini nchini Ujerumani wakitaka askofu huyo afukuzwe kazi.
Miongoni mwa matumizi yake makubwa ni
ujenzi wa makazi yake binafsi yaliyogharimu Euro 2.9 milioni (Dola 3.9
milioni), ukumbi wa chakula wenye mita za mraba 63 ambao ni pamoja na
mesi na bafu yenye thamani ya Euro 15,000.
Askofu van Elst (53) amekuwa
akituhumiwa kuendesha miradi hiyo kwenye mji wa kihistoria wa Limburg,
ikiwamo makumbusho, kumbi za mikutano, kanisa dogo na nyumba ya makazi
yake binafsi.
Fedha hizo zinatokana na mapato ambayo ni misamaha ya kodi kwa vikundi vya kidini nchini Ujerumani kwa mujibu wa sheria.
"Baada ya uchunguzi wa awali, Vatican
imeamua kuchukua hatua kumsimamisha na kumwondoa kwenye usimamizi wa
jimbo," ilieleza taarifa hiyo.
"Baba Mtakatifu (Francis) amekuwa
akifuatilia kwa karibu mambo yote yanayoendelea katika Jimbo la
Limbuerg," iliongeza taarifa hiyo.
"Hali hiyo imefikia mahali ambako kiongozi huyu hawezi kuendelea kusimamia kazi zake za kitume kama askofu wa jimbo."
Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza ni
kwa muda gani Askofu van Elst amesimamishwa kazi, ila iliongeza kuwa
itategemea na kukamilika kwa uchunguzi, tathmini ya hali ya fedha ya
jimbo na mambo mengine.
Wiki iliyopita, Askofu van Elst
alisafiri hadi mjini Rome, Italia kwa ndege ya shirika la gharama nafuu,
Ryanair kujieleza mbele ya Papa Francis – kutokana na madai kuwa
alisafiri mwaka jana kwa ndege ya daraja la kwanza kwenda India na pia
kutumia vibaya fedha.
Taarifa za matumizi hayo makubwa ya
kiongozi huyo zimelitikisa Kanisa Katoliki la Ujerumani huku wengi
wakitaka uwazi katika matumizi ya fedha -- mageuzi ambayo Papa Francis
amekuwa akiyapigia kelele na kutaka kanisa maskini kwa watu maskini.
Miradi hiyo kwa pamoja ambayo iliidhinishwa na mtangulizi wake awali
ilikadiriwa kutumia Euro 5.5 milioni, lakini iliongezeka kwa kiasi cha
kutisha na kufikia Euro 31 milioni ikiwamo bustani yenye thamani ya Euro
783,000.
Pia, Askofu Tebartz-van Elst
anatuhumiwa kwa kutoa taarifa za uongo mahakamani kuhusu safari yake ya
India kutembelea familia maskini.
Waendesha mashtaka wa Serikali
wanaeleza kuwa askofu huyo alitoa taarifa za uongo chini ya kiapo kwenye
mahakama ya mjini Hamburg dhidi ya gazeti la kila wiki, Der Spiegel
akikana safari ya India anakodaiwa kutumia daraja la kwanza. Matumizi
makubwa ya askofu huyo yameudhi walipa kodi wa Ujerumani wakidai kwamba
wanakamuliwa huku fedha zikitumiwa vibaya na wengi wao kuandamana nje ya
makazi ya askofu huyo.
Kansela Angela Merkel, binti wa
kiongozi wa zamani wa Kipentekoste amesema kupitia msemaji wake, Steffen
Seibert kwamba ana matumaini Kanisa Katoliki litamaliza tatizo hilo kwa
jina la Yesu. Askofu Tebartz-van Elst hata hivyo ametetea miradi yote
akieleza inalenga kudumisha mila na historia ya eneo hilo.
Tangu kuingia madarakani kwa Papa Francis, kumekuwa na kasi ya mabadiliko ndani ya kanisa.
No comments:
Post a Comment