KUNDI la waasi wa M23, linalopambana
na Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
limetajwa kuwa chanzo cha kuisambaratisha Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC). Kauli hiyo imetolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, katika mahojiano yake na kituo
cha redio cha Clouds.
Membe amesema kinachosababisha
Tanzania itengwe na baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya ya EAC, ni hatua
yake ya kupeleka majeshi katika mji wa Goma ulio Mashariki mwa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa ajili ya kupambana na waasi
wanaoipinga Serikali ya Rais Joseph Kabila.
Amesema hatua hiyo ya Tanzania
ilizikera baadhi ya nchi wanachama wa EAC, zenye maslahi ya moja kwa
moja na kundi hilo na kusisitiza kuwa hata kama itatengwa, kamwe
haitaondoa vikosi vyake DRC na badala yake vitaendelea kupambana.
"Najua sababu za wenzetu kuharakisha
shirikisho la kisiasa na kuamua kufanya vikao vya siri vya kuitenga
Tanzania, ni uamuzi wetu wa kupeleka vikosi vya kijeshi Congo,
wanalalamika kwamba ni kwanini tumefanya hivyo na kudai kuwa maamuzi
yetu hayo yatauvunja umoja wetu, sisi tukawaambia hatuwezi kuacha kuleta
amani Kongo, hiyo ndiyo sababu," alisema Membe.
Aliitaja sababu nyingine inayotishia
uhai wa jumuiya hiyo kuwa ni uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kukataa suala
la ardhi kuingizwa katika mambo ya pamoja ya jumuiya.
"Sisi ni nchi kubwa, tuna kila kitu,
tuna ardhi kubwa, hatuendeshi nchi yetu kwa muungano wa makabila,
wenzetu wanatuonea wivu, wanaitaka ardhi yetu, Mzee Kikwete amekataa,
wanaamua kututenga, niwahakikishie Watanzania, hatuna hofu hata chembe
na suala hili.
"Hawa jamaa pia wanakerwa na hatua
yetu ya kuwepo kwenye Jumuiya ya SADC, wanaona kama tunafaidi sana,
lakini niwaambie kwamba hatuwezi kutoka SADC, mbona wao wako COMESA,"
aliongeza Membe.
Aidha Membe aligusia ujio wa viongozi
wa Kimataifa nchini Tanzania kuwa moja ya sababu za nchi wanachama wa
EAC kuitenga Tanzania, kwa madai kuwa inafanya mambo yake yenyewe.
Kwa miezi kadhaa kumekuwa na jitihada
zinazofanywa na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda za kutaka kuunda
shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki pasipo kuishirikisha Tanzania.
Tayari marais hao wamekwishaanzisha
mipango ya pamoja ya kiuchumi na kuimarisha miundombinu ya reli na
bandari, ambapo mwezi Agosti mwaka huu walikutana mjini Mombasa kwa
ajili ya uzinduzi wa gati namba 19 la kuingiza na kutoa mizigo katika
Bandari ya Mombasa.
Taarifa nyingine za hivi karibuni
kutoka nchini Rwanda zimeeleza kuwa nchi hizo tatu zimekwishaunda kikosi
kazi kilichopewa jukumu la kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho la
Afrika Mashariki. Chanzo: Rai
No comments:
Post a Comment