Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni jana jioni walitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge, baada ya kupuuzwa kwa mwongozo wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa.Wabunge waliotoka bungeni jana yapata saa 12.15 ni kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi huku Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP, Augustine Mrema akiendelea kubaki ukumbini.
Kitendo cha wabunge hao wa upinzani
kilionekana kuwakera baadhi ya wabunge wa CCM, ambao walisikika
wakiwakejeli kwa kupiga meza huku wakisema: "Kwendeni zenu, tumewazoea."
Wakati wabunge hao wakiondoka, Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikuwa akiwasisitiza wabunge wanaobakia
wawe watulivu, maana kuna usalama wa kutosha ndani ya ukumbi huo.
"Mnaotoka nimewaona wote na mnanijua," alisikika Naibu Spika Ndugai akiwatahadharisha wabunge wa upinzani waliosusa mjadala huo.
Wabunge wa CCM waliendeleza vituko
ambapo baada ya wapinzani kutoka, wabunge Juma Nkamia (Kondoa Kusini),
Hilary Aeshi ( Sumbawanga Mjini) na Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini)
walikwenda kukaa katika viti vya kambi ya upinzani.
Kabla ya kutoka kwa wabunge hao
wabunge wawili kutoka CUF waliomba mwongozo wa Spika, wakitaka muswada
huo kuondolewa ili kuwapa nafasi Wanzanzibar kutoa maoni yao.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed
Mnyaa (CUF) aliomba mwongozo akitaka muswada huo uondolewe, hadi hapo
Wazanzibar watakaposikilizwa.
Alisema kuwa kwa maoni ya Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala wamesikiliza maoni ya wadau wengi, lakini
Zanzibar hawakwenda kuwasikiliza wadau wa eneo hilo.
"Na hili suala zima katika masuala ya
katiba linahitaji usawa wa washirika, tunazungumza kitu kinachohusiana
na Zanzibar na Tanzania Bara, ili kupata maoni ya nchi nzima kuna
uhalali gani wa Bunge hili kuendelea na mjadala huu?" alihoji.
Hata hivyo, alikatizwa na kelele za
Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM), ambaye alitoa taarifa kuwa
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilialika wajumbe mbalimbali ikiwamo
Zanzibar. Tembelea http://jambotz8.blogspot.com/ kila siku.
"Miongoni wa wajumbe walioalikwa ni
pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na
wadau mbalimbali ambao walikuja mbele ya Katiba," alisema Pindi ambaye
pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Mbunge wa Konde, Khatibu Said Alli
(CUF), alitaka mwongozo wa Spika kuhusiana na ujumbe mfupi wa maneno
ambao aliupokea ukimtisha, kutokana na kitendo chao cha kumuunga mkono
Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu.
"Unashabikia mambo ya Tundu Lissu leo,
endelea ila mtashughulikiwa," aliunukuu ujumbe huo na kuongeza kuwa
hafahamu umetoka kwa mbunge gani ila wahudumu wa Bunge ndio
waliompelekea.
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema
kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo anayachukua na kuyafanyia kazi ni
suala hilo. Pia Ndugai aliomba ujumbe huo apelekewe.
"Hii ni demokrasia mara nyingi
imeshatolewa miongozo, jibu linatolewa hapo hapo ama baadaye na kwa hoja
zilizotolewa inakilazimu kiti kupata ushauri hapo baadaye," alisema
Ndugai. Tembelea http://jambotz8.blogspot.com/ kila siku.
Hata hivyo, baada ya Ndugai kutoa majibu hayo, wabunge wa upinzani waliamua kutoka ndani ya ukumbi huo.
Baada ya wabunge hao kutoka Naibu
Spika Ndugai aliendelea na ratiba ya Bunge kwa kusema, jambo hilo
halikupangwa kumalizika jana na kwamba litaendelea kujadiliwa hata
ikibidi hadi keshokutwa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama
kabla ya mjadala kuendelea na kutetea hoja kuwa makundi yote
yalisikilizwa tofauti na inavyodaiwa na wapinzani.
"Hata katika marekebisho ya sheria
mbili hizi, mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumekutana na viongozi
wengi na mawaziri na ndiyo maana tumeahirisha Muswada wa Sheria ya Kura
ya Maoni," alisema.
Alisema, yeye (Lukuvi) alikuwa
Mwenyekiti wa ujumbe uliotumwa na Rais kuitisha makundi ya siasa ambayo
yalijadili muswada huo. Lukuvi alisema kuwa, pande zote zimeshiriki
kikamilifu katika kutoa maoni yao, "kama hizi ni sarakasi za kisiasa
mimi sijui."
Baada ya kutoka, wabunge wa vyama vya
Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walifanya mkutano wa pamoja kwenye Ukumbi
wa Pius Msekwa. Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa,
wabunge hao walikubaliana kufanya kila njia kuhakikisha wanazuia mjadala
huo leo.
Pia wabunge wa CCM nao walikutana nao mara baada ya Ndugai kuahirisha kikao cha jioni.
Lissu achafua hali ya hewa
Hotuba ya Lissu ndiyo iliyochafua hali
ya hewa baada ya kuituhumu Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
kwa kutohoji watu wa Zanzibar wakati wakikusanya maoni kuhusu muswada
huo.
Alisema licha ya kamati hiyo kukusanya
maoni ya taasisi za kidini na za kiraia, taasisi za elimu ya juu na za
kitaaluma, vyama vya siasa na asasi nyingine, lakini bado haikwenda
Zanzibar kukusanya maoni ya watu wa huko.
"Wadau pekee walioshirikishwa kutoa
maoni yao juu ya muswada huu ni Watanzania Bara tu. Wazanzibari
hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya sheria
yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar," alisema Lissu.
Pamoja na suala hilo, Lissu alitaka
pia Rais wa Jamhuri ya Muungano aondolewe madaraka ya kuteua Wajumbe wa
Bunge Maalumu wasiokuwa wabunge au wawakilishi kuwa inavuruga au kuondoa
kabisa dhana ya uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika
mchakato wa Katiba Mpya. Tembelea http://jambotz8.blogspot.com/ kila siku.
Pia alipendekeza kuongezwa kwa idadi
ya wajumbe ifikie 792, kwani Tanzania ina idadi ya watu milioni 45 kwa
takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Lissu pia alitaka wawakilishi wa
Zanzibar waongezwe bungeni, kwa Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 kwenye
Bunge lenye wajumbe 604, sawa na takriban 36% ya wajumbe wote. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka idadi iwe nusu kwa nusu kati ya pande
mbili za Muungano.
Wajumbe 166
Kutakuwa na wajumbe 166 wasiotokana na
Bunge na Baraza la Wawakilishi watateuliwa na Rais. Kutakuwa na Wabunge
357 na Wawakilishi 81 na kufanya Bunge Maalumu kuwa na jumla ya wajumbe
604.
Chikawe asoma muswada
Mapema akisoma muswada huo, Waziri wa
Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alisema Rais atakaribisha makundi
mbalimbali kuwasilisha majina yasiyozidi matatu kila kundi ambao
watateuliwa kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Alisema pia Kifungu
cha 27 (2) kitatoa fursa kwa uhuru wa maoni katika mijadala ya Bunge
Maalumu na maoni hayo hayatahojiwa mahakamani au sehemu yoyote nje ya
Bunge Maalumu.
Chikawe alisema Bunge Maalumu la
Katiba litakaa kwa siku 70 mfululizo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kujadili rasimu hiyo. Hicho kitakuwa kikao kirefu zaidi cha Bunge kuwahi
kukaa nchini Tanzania.
"Kutokana na unyeti wa suala lenyewe
muswada huo unampa nguvu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
kuongeza siku 20 ili kujadili katiba," aliongeza Chikawe.
Imeandikwa na Daniel Mjema na Sharon Sauwa
No comments:
Post a Comment