WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imeanza kushughulikia utaratibu wa
kurejesha utoaji wa elimu ya kidato cha kwanza hadi kidato cha nne
katika baadhi ya shule kongwe ili kurudisha ufaulu uliokuwepo na
kuimarisha malezi ya watoto kuanzia elimu ya chini.
Amesema
uamuzi huo unafuatia kaulimbiu ya kutaka kuwajengea wanafunzi maadili
mema katika mazingira ya shule za sekondari tangu wanapoingia kidato cha
kwanza badala ya mfumo wa sasa ambapo wanakuja kupata mafunzo hayo
kidato cha tano na cha sita lakini wanakuwa hawajapata msingi imara
tangu wakiwa wadogo.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Septemba 21, 2013) wakati akizungumza
na mamia ya wanajumuiya waliohitimu katika shule hiyo (Alumnae),
wanafunzi waliopo pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe za
Jubilei ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, alikuwa akijibu
maombi yaliyotolewa na Dk. Maria Kamm ambaye aliongoza shule hiyo kwa
miaka 22 kuanzia mwaka 1970 hadi 1992, pamoja na wazungumzaji wengine
katika sherehe hizo.
Alisema
Serikali ilikwishatoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kwa ajili
ya shule tano ambazo ziliondolewa madarasa ya kidato cha kwanza hadi cha
nne na mojawapo ya shule hizo ni Sekondari ya Wasichana ya Weruweru.
“Taarifa
za awali zinaonyesha kuwa Weruweru ina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa
kidato cha kwanza wakati wale waliopo wakiendelea na masomo yao. Tatizo
litakuwa ni kwamba hamtaweza kuanza na mchepuo zaidi ya mmoja,” alisema
huku akishangiliwa.
Alisema
mbali ya kigezo hicho, Serikali iliangalia pia shule zinazotaka
kurudishiwa mpango huo kama zina eneo la kutosha kuongeza majengo na
ikabaini kuwa shile hiyo ya Weruweru inalo eneo la kutosha. “Jambo hili
linawezekana, kwa hiyo tutaangalia taratibu zilizopo zikamilike mapema
na shule hii ianze kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza, na mwaka
unaofuata wa kidato cha pili hadi tukamilishe,” aliongeza.
Waziri Mkuu alisema uamuzi huo umelenga pia kutekeleza Ibara ya 85 ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza kwamba udahili wa wanafunzi wa kike katika Vyuo Vikuu ufikie asilimia 40 ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka.
“Nia ya Serikali ni kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika Vyuo Vikuu hadi kufikia asilimia 40. Lakini ili kufikia hapo ni lazima kuwe na idadi kubwa ya wanafunzi waliohitimu ili kupata mnyororo uliokamilika. Lazima kuwe na muendelezo wa wahitimu wengi zaidi,” alisema.
Alisema
hivi sasa idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari nchini kote ni
1,884,272 ambapo kati yao wasichana ni 873,799 sawa na asilimia 46.4
wakati wavulana ni 1,010,473 sawa na asilimia 53.6.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alibainisha kwamba Tanzania hivi sasa ina vyuo vikuu
45 (vya serikali ni 14 na biafsi ni 31) ambavyo vina wanachuo wapatao
166,484 wakiwemo wanawake 60,592 (sawa na asilimia 36.4) na wanaume
105,892 (sawa na asilimia 63.6).
Mapema,
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philip Mulugo alisema
Serikali iliondoa mfumo wa kidato cha kwanza hadi cha nne katika baadhi
ya shule ili kukabiliana na hitaji la shule nyingi za kidato cha tano
baada ya kuanzishwa kwa shule za kata ambazo nyingi zina kidato cha
kwanza hadi cha nne tu.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu aliahidi kuisaidia shule hiyo kufanya harambee ili iweze
kutimiza ndoto yake ya kukusanya sh. milioni 500 za kufanya ukarabati wa
majengo ya shule hiyo kongwe.
“Nimemwambia
Mwalimu Mkuu pamoja na kamati ya harambee, andaeni mchanganuo juuya
nini hasa mnataka kifanyike kwa ajili ya ukarabati. Onyesheni kila
darasa, maabara ama bweni litagharimu kiasi gani. Onyesheni vipaumbele
vyenu halafu mniletee. Mimi nitachukua fursa ya kuomba mtu mmoja mmoja
kwa maandishi ili watusaidie kukamilisha kazi hii nzuri ambayo
mmeianza,” alisema.
“Tujipange
upya kuona tunataka Weruweru ya namna gani, tunataka shule hii iweje
miaka 50 ijayo… hakuna kurudi nyuma katika hili mliloazimia kulifanya.
Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, mmetoa wahitimu 12,757 kutoka
shule hii. Hii si idadi ndogo. Ni lazima tuhakikishe sifa ya Weruweru
haipotei lakini kikubwa ni kuazimia kwa pamoja kwamba tunataka Weruweru
ibadilike irudie enzi zake ilipokuwa ikitamba na kutoa watoto wengi
waliofaulu kwa alama za juu,” alisema.
Katika
harambee ya papo kwa papo, Waziri Mku alifanikiwa kuchangisha sh.
milioni 62.6/- zikiwa ni fedha taslimu na ahadi. Hata hivyo, wana Alumnae
wa Weruweru walikuwa wamekwishakusanya michango mingine ya ahadi na
fedha taslimu na kufanya jumla ya michango yote kufikia sh. milioni
104.6/-.
Baadhi
wa wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo ni Dk. Asha-Rose Migiro, Dk.
Mary Nagu, Balozi Mwanaidi Maajar, Bi. Anna Kilango Malecela, Dk. Mwele
Malecela, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Hajat Amina Mrisho na wengine wengi
ambao wameshika nafasi mbalimbali za uongozi katika mashirika, taasisi
na Serikalini.
No comments:
Post a Comment