MAMA ANNA MKAPA.
MKUTANO
wa wake za marais uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na viongozi wazito, akiwemo Rais wa zamani wa Marekani,
George W. Bush na Mkewe, Laura, umeacha kitendawili kizito kuhusu mke wa
Rais wa zamani, Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa. Imebainika kuwa katika
mkutano huo, ambao mke wa Rais Jakaya Kikwete, Salma alikuwa ni
mwenyeji wao, Mama Anna Mkapa hakuhudhuria, lakini pia imeonyesha wazi
kwamba hakupewa fursa kulingana na hadhi yake.
Mkutano
huo wa Kimataifa ulifanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es
Salaam, Juni 2-3 mwaka huu, uliozungumzia nafasi ya wanawake kuinuka
kimaendeleo, ukizihusisha taasisi zinazoendeshwa na wake wa marais,
wakiwemo wale wastaafu.
Gazeti moja hapa nchini lilibaini kuwa,
katika mkutano huo kiligawiwa kitabu kilichobeba jina la ‘African First
Ladies Summit’, kilichokuwa na orodha ya viongozi mbalimbali, wakiw
emo
wake za marais na wake za marais wastaafu takribani 31, kikielezea
wasifu na taasisi wanazoziongoza, lakini Jina la Mama Mkapa halikuwemo.
Katika
kitabu hicho, Mama Mkapa, ambaye anaendesha Taasisi ya Fursa Sawa Kwa
Wote (EOTF), jina lake kutokuwepo, baadhi wanaona kwamba Mkutano huo
haukumpa fursa mama huyo, hasa kutokana na kazi kubwa ambayo imekuwa
ikifanywa na taasisi yake hiyo ya kuwainua wanawake kama mazungumzo ya
mkutano huo yalivyokuwa yameegemea.
Taasisi ya EOTF ni taasisi ya
kwanza kuendeshwa na mke wa Rais hapa nchini, na ilianzishwa wakati Rais
Benjamin Mkapa akiwa madarakani. Tangu ilipoanzishwa imekuwa
ikijishughulisha na kuwainua wanawake kiuchumi kupitia shughuli
mbalimbali, ikiwemo ujasiriamali.
Tofauti na mama Anna Mkapa ambaye
haijulikani kama alitengwa au alijitenga katika mkutano huo, lakini
kitabu hicho kilielezea wasifu na shughuli zinazofanywa na wake za
marais kama Mama Salma kupitia taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA), Mke wa Rais Obama, Michelle ambaye juhudi zake amezielekeza
katika kujenga jamii na familia kupitia mradi wake wa Let’s Move!.
Wengine ni pamoja na mke wa Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair, Cherie Blair, Laura Bush na wengine.
MTANZANIA Jumapili lilimtafuta
kwa njia ya simu msaidizi wa Mama Mkapa aliyetambulika kwa jina moja la
Prisca, ambaye alikiri kuwa alipata mwaliko wa mkutano huo.
Kuhusu kutohudhuria, alisema hilo
lilitokana na programu zake nyingi, ikiwa ni pamoja na banda ndani ya
viwanja vya maonyesho ya kimataifa ya 37 ya biashara, Sabasaba ambako
alikuwa na wageni wake.
Alipoulizwa mbona mkutano huo ni
mkubwa sana huku Mama Salma pia akiwa na banda lake huko, lakini
aliliacha na kwenda katika Mkutano, iweje kwa mama Mkapa, Prisca alisema
hilo limetokana na kuwa na ‘programu’ zake nyingine.
Prisca alipoulizwa kama Mama
Mkapa alialikwa katika mkutano huo, alisema kualikwa si tatizo, kwani
anaweza kualikwa, lakini akawa na mambo mengine.
Alipoulizwa kama kuna tatizo kati
ya EOTF na WAMA, alieleza kuwa hakukuwa na tatizo lolote, kwani hata
katika kumpokea Mama Obama wakati alipotembelea ofisi za WAMA, Mama Anna
Mkapa alikuwepo.
Prisca alisema kuwa hakuna tatizo
kwa kuwa Mama Salma ni mke wa rais na Mama Mkapa alikuwa mke wa rais,
hivyo hawana cha kugombea.
“Mama Salma akimwita Mama (Anna) kwenye ‘programu’ zake huwa anakwenda, vivyo hivyo kwa mama anapomwita mama Salma.
“Ninyi waandishi mambo
madogomadogo kama hayo muwe mnayaacha na ndiyo yanawaweka katika
matatizo na familia zenu, Mama Salma na Mama Mkapa wote wako ‘busy’ na
hivi vitu naomba viishie hapo… kwanza umepata wapi namba yangu?” Alihoji
Prisca.
Mkutano huo wa wake za marais,
mbali na kuhudhuriwa na mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza,
Cherie Blair, ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kupambana na Ukimwi (Unaids), Michel Sidibé.
Baadhi ya wake za marais
waliohudhuria pia ni pamoja na Mke wa Rais wa Uganda, Janet Museveni,
mke wa Rais wa Msumbiji, Maria da Luz Dai Guebuza, mke wa Rais wa Sierra
Leone, Sia Nyama Koroma, Balozi Nancy G. Brinker ambaye ni kiongozi wa
kimataifa wa kupambana na ugonjwa wa kansa pamoja na wengine wengi.
No comments:
Post a Comment