TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Afanya ziara ya kushtukiza kwenye kambi ya wajenzi wa Kichina
*Aahidi kumtuma Waziri Magufuli kufuatilia, ataka mkandarasi aongeze kasi, awe makini
*Amtaka RC Rukwa aunde timu ya kumpatia ripoti kila mwezi
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda jana jioni (Jumamosi, Juni Mosi, 2013) alilazimika
kufanya ziara ya ghafla kwenye kambi ya wajenzi wa barabara ya
Kanazi-Kizi-Kibaoni ili kupata maelezo ni kwa nini kazi hiyo inasusua na
haionyeshi kuendelea.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa akitoka Namanyere, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa
ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya
Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yanafanyika mkoani Rukwaalilazimika kusimama kwenye kambi hiyo ya wajenzi iliyopo Paramawe, wilayani Nkasi.
Kampuni
inayohusika na ujenzi wa barabara hiyo ni China Hunan Construction
Engineering Group Corporation (CHCEG) na gharama za mradi huo ni sh.
bilioni 82.8/- ambapo hadi sasa kiasi cha sh. bilioni 16.37
kimekwishatolewa na Serikali kwa mkandarasi huyo.
Barabara
hiyo ya kutoka Kanazi kupitia Kizi hadi Kibaoni ambayo ina urefu wa km.
76.6, ilianza kujengwa Juni 2009 na ilipaswa kuwa imekamilika Machi
20, mwaka huu lakini hadi sasa haijawekewa hata kilometa moja ya lami.
Ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya pili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda kupitia Namanyere.
Akitoa
maelezo mbele ya Waziri Mkuu, Meneja wa TANROADS mkoa wa Rukwa,
Mhandisi Florian Kabaka alisema mradi huo uliokuwa umepangwa kukamilika
katika kipindi cha miezi 36, unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo
vipindi virefu vya mvua (Desemba – Mei) na kukosekana kwa wataalamu
waliobobea kwenye kazi hiyo.
“Awali
mradi huu ulikuwa umepangiwa miezi 36 na ulipaswa kuwa umekamilika
tangu mwezi Machi lakini kulizuka ubishi wa tarehe ya kuanza mradi na
kukawa na tatizo la kukosekana wataalamu wenye sifa zinazostahili pamoja
na vipindi virefu vya mvua,” alisema.
Alisema
tatizo jingine lililoukumba mradi huo ni mkandarasi kuwa anasimamisha
kazi kila mara kwa sababu ya ukosefu wa fedha licha ya kuwa amekuwa
akilipwa kwa awamu. “Fedha amekuwa akilipwa kwa awamu lakini alipaswa
kutumia hata fedha zake ili kuhakikisha kuwa kazi inakamilika katika
muda uliopangwa kwenye mkataba,” alisema Bw. Kabaka.
Alipoulizwa
na Waziri Mkuu ni wataalamu gani ambao hawajapatikana, Mhandisi Kabaka
aliwataja kuwa ni Meneja Mradi, Mhandisi wa Maabara na Mhandisi wa
Barabara.
Naye
Mkandarasi wa kampuni ya CHCEG, Bw. David Shi Weiwe alipotakiwa na
Waziri Mkuu atoe maelezo juu ya kusuasua kwa mradi huo alisema baada ya
kufanya mazungumzo na wakuu wa TANROADS wiki iliyopita huko Dar es
Salaam, wameahidi kukamilisha taratibu za kuwapata wataalamu
wanaohitajika. Hata hivyo, alisema wanakwamishwa na utaratibu wa
upatikanaji wa viza ambao unaweza kuchukua karibu miezi miwili.
Waziri
Mkuu alisema miezi miwili ni mingi na akamtaka mkandarasi huyo
awasiliane na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya endapo
kuna vikwazo watakumbana navyo katika kukamilisha kazi yao. Alisema
atamwagiza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akazuru maeneo yote ya
ujenzi kuanzia Tunduma hadi Mpanda yakiwemo Sumbawanga na Laela.
Pia
alimtaka aongeze kasi ya ujenzi huku akizingatia umakini katika kipindi
cha miezi mitano ijayo ambacho hakina mvua ili kukamilisha kilometa 16
za lami ambazo ameahidi mbele ya Waziri Mkuu kwamba zitakuwa tayari
ifikapo Novemba, mwaka huu.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu huyo wa Mkoa aunde timu ndogo ya watu
watano wakiwemo watu wa TANROADS itakayokuwa inafuatilia kazi ya ujenzi
wa barabara hiyo pamoja na ile ya Sumbawanga – Matai – Kasanga na kumpa
taarifa aiwasilishe kwa Waziri Mkuu kila mwezi juu ya maendeleo ya
ujenzi wa barabara hizo mbili.
“Hamuwezi
kukaa na kusubiri maamuzi ya kikao cha RCC ambacho ratiba yake ni
kukutana mara mbili kwa mwaka. Tumia timu hii ndogo, hakikisha
inafuatilia kwa karibu na kutupa taarifa ya nini kinafanyika kila mwezi,
nataka tuone katika miezi mitano ijayo tutafikia wapi,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JUNI 2, 2013.
No comments:
Post a Comment