Wednesday, June 05, 2013

KESI DHIDI YA RUTO KUHAMISHIWA KENYA AU TANZANIA

 Nairobi, Kenya. Kesi inayomkabili makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huenda ikahamishiwa nchini Tanzani au Kenya.
Hiyo inatokana na uamuzi unaotajwa kufikiwa na majaji wa ICC ambao wametoa mapendekezo wakimtaka Rais wa ICC aangalie umuhimu na kutoa ruhusa ya kesi hiyo kusikiliziwa nchini Kenya au kama ikishindikana basi isikiliziwe nchini Tanzania.
Uamuzi huo unaweza pia kusababisha athari za kuichochea mahakama hiyo kuhamisha pia kesi ya aina hiyo inayomhusu Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia mawakili wake wameomba kesi dhidi yake ihamishiwe nchini Kenya au Tanzania.
Ruto pamoja na mtuhumiwa mwenzake, aliyekuwa mtangazaji wa Redio, Joshua Arap Sang wanakabiliwa na mashtaka kadhaa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu wakidaiwa kuhusika kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.
Mapendekezo hayo yametokana na ombi hilo lililotumwa Januari 24 mwaka huu ambalo lilikuwa bado likiendelea kujadiliwa n amamlaka zinazohusika kwenye mahakama hiyo.
Februari mwaka huu, Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda aliieleza mahakama hiyo kwamba hana pingamizi iwapo itakubalika kesi hiyo isikiliziwe Tanzania au Kenya.
Hata hivyo mahakama hiyo ilieleza kuwa mapendekezo hayo bado yanaendelea kujadiliwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mahakama hiyo.
Hata hivyo, jana ICC ilitoa taarifa ikisema kesi dhidi ya Ruto anayetuhumiwa kufanya makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu itaanza Septemba 10 mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema majaji wameamua kupanga tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo mapema zaidi kuliko ilivyopangwa awali.
Rais Kenyatta na naibu wake wanahitajika kupandishwa kizimbani ili kujibu mashtaka yanayowakabili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, makosa ambayo waliyafanya wakati wa vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Rais wa mwaka 2007/08.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...