Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda (wa tatu kulia) akiwasili jana.
MWENYEKITI
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda amerejea chini
jana kutoka Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa na kusisitiza kwamba
hatanyamaza kuzungumzia janga la kushambuliwa kwake.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege
wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Kibanda alisema asingependa kuona
jambo hilo linamtokea mwandishi mwingine wa habari.
Kibanda,
ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd,
alikuwa akitibiwa huko baada ya kushambuliwa na kuumizwa vibaya na watu
wasiofahamika usiku wa Machi 5, mwaka huu.
Alisema kutokana na hali hiyo, waandishi wanapaswa kuwa na mshikamano ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayajirudii.
“Waandishi
wana nafasi kubwa ya kuliondoa taifa katika hali hii. Waendelee
kuandika na kuelimisha wananchi ili nao wasaidie kuzuia ukatili wa aina
hii. Hatuwezi kuishi katika nchi ambayo watu wanafanyiwa ukatili
mkubwa kiasi hiki halafu wanaachwa hivihivi,” alisema Kibanda.
Kibanda alisema jambo lililomtokea lilikuwa baya kwani alikuwa akipoteza fahamu kila wakati kutokana na maumivu makali.
“Lakini
sasa namshukuru Mungu, nimepona, sina maumuvu tena kama yale,” alisema
Kibanda na kuelezea kufurahishwa kwake na ushirikiano mkubwa alioupata
kutoka kwa wadau wa habari na wananchi kwa jumla.
Ameiomba
Serikali kuharakisha ripoti ya uchunguzi wa tukio lake kwa sababu ni
muda mrefu umepita na kwamba mpaka sasa hakuna taarifa zozote
zilizotolewa.
“Nilipolazwa
Muhimbili Kitengo cha Moi, alikuja kuniangalia Kamanda wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Mkuu wa Jeshi la Polisi,
Said Mwema waliniahidi kushughulikia suala langu ili waliohusika na
tukio hili wafikishwe mahakamani,” alisema.
Alisema
si hao tu, bali pia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, ambaye alikwenda Afrika Kusini kumjulia hali, alimwahidi
kuwashughulikia watu waliohusika.
“Sisi
sote ni mashahidi wa ukimya ambao upo kwani mpaka sasa watu hao
hawajakamatwa, wala hakuna taarifa zozote zinazohusu kufikishwa
mahakamani,” alisema.
Kibanda
alisema katika miaka ya karibuni, kumekuwa na matukio mbalimbali
yanayohusisha kupigwa, kuuawa au kutishiwa maisha kwa waandishi, jambo
ambalo linaonyesha wazi kuwa matukio hayo hayaji bure, kuna chanzo
chake.
No comments:
Post a Comment