Friday, May 24, 2013
POLISI ALIEKAMATWA NA GUNIA ZA BANGI ATOKOMEA KIZANI NA WALE WALIOKAMATWA NA FUVU NAO VILE VILE
Na Eliya Mbonea, Arusha
ASKARI Polisi Koplo Edward, anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya (bangi) gunia 18 ametoroka chini ya ulinzi wa askari polisi saba na kutokomea kusikojulikana. Mtuhumiwa huyo, alikuwa dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser namba PT. 2025 la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana, kwamba askari huyo akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi saba, walikwenda nyumbani kwake kwa ajili ya ukaguzi.
Alisema wakiwa nyumbani kwa mtuhumiwa, waliingia ndani kuendelea na upekuzi, lakini katika mazingira ya kutatanisha aliwatoroka na kukimbia bila kufanikiwa kumkamata.
Alisema kutokana na hali hiyo, polisi mkoani Arusha limemkamata Inspekta wa Polisi Izaack Manoni aliyekuwa anasimamia upekuzi huo.
“Inspekta Manoni yupo chini ya ulinzi na hatua za kinidhamu dhidi yake zitachukuliwa,” alisema ACP Sabas na kuongeza:“Mtuhumiwa Edward, anayetafutwa kwa sasa alishafukuzwa kazi, akipatikana atafikishwa mahakama ya kiraia kusomewa mashitaka ya kufanya biashara ya dawa za kulevya,” alisema.
Mei 18, mwaka huu saa 5 usiku eneo la Himo, polisi wa Kilimanjaro walikamata gari la polisi lenye namba PT 2025, likiwa limesheheni magunia 18 ya bangi likielekea Holili, karibu na mpaka wa Kenya.
Alisema tayari mtuhumiwa mwenzake ambaye ni askari polisi mwenye namba G. 2434 PC George, amesomewa mashitaka yake jana. Mbali na mtuhumiwa huyo, watuhumiwa wengine waliokamatwa na magunia 30 ya bangi wilayani Arumeru nao wamepandishwa kizimbani kusomewa mashitaka yao.
Taarifa kutoka eneo la Kwa-Morombo ilipo nyumba ya mtuhumiwa aliyetoroka, zilidai baada ya kufika nyumbani kwake, askari saba waliiongozana naye walimuamini na kumwacha kuingia ndani peke yake.
Ilidaiwa baada ya kuingia ndani, mtuhumiwa huyo alifungua mlango wa nyuma ya nyumba yake na kutoroka, huku askari waliokuwa wakisimamia upekuzi huo wakipigwa butwaa kutokumuona mtuhumiwa wao akitoka nje. Hakuna kiongozi wa jeshi la polisi, au Serikali mkoani Mtwara ambao walikuwa tayari kuelezea tukio hilo hadi tunakwenda mitamboni.
Morogoro
----------
Na Rose Chapewa, Morogoro
Habari kutoka mkoani Morogoro, zinasema askari polisi watatu mkoani humo, waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kumbambikizia kesi ya kukutwa na vufu la kichwa cha binadamu mfanyabishara Samsoni Mwita, mkazi wa Dumila, wamefukuzwa kazi.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, ilisema hatua ya kuwafukuza askari hao ilifikiwa baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema katika uchunguzi huo, ilibainika askari hao walikwenda kufanya upekuzi kwa mfanyabiashara huyo, bila kuwa na kibali cha maofisa wao wa kazi.
Aliwataja askari hao, kuwa ni mwenye namba D 4807 D/Stafu Sajenti (SSGT) Sadick wa kituo kidogo cha Polisi Dakawa, E 4344 Sajenti (SGT) Mohamed na E 3821 Koplo (CPL), Nuran wote wa kituo kidogo Dumila.
Alisema askari hao, walifanya tukio hilo Mei 7, mwaka huu, saa 5 asubuhi katika kijiji cha Mgudeni, Dumila wilayani Kilosa, ambapo walimbambikizia kesi ya kukutwa na fuvu la kichwa kinachodaiwa kuwa cha binadamu mfanyabiashara huyo kwa lengo la kujipatia fedha.
Alisema askari hao walifanya hivyo kwa makusudi, huku wakijua kuwa ni kosa kisheria kwa askari polisi yeyote kumbambikizia kesi raia na ni kunyume cha taratibu, sheria, kanuni na maadili ya jeshi hilo.
Alisema katika uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo, umebaini askari hao wamefanya kitendo hicho kwa kushirikiana na raia Rashidi Ally (47), mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaamu.
Awali ilidaiwa kuwa nia ya askari hao kumbambikizia kesi ya fuvu mfanyabiashara huyo, ilikuwa kujipatia Sh milioni 25 kwa njia ya utapeli.
MTANZANIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment