JESHI la polisi limekumbwa na kashfa nyingine baada ya askari wake kudaiwa kumpiga risasi msichana wa miaka 16 baada ya kumkuta akivunja amri ya sita ndani ya gari.
(Jina tunalihifadhi) alikumbana na mkasa huo Jumatano usiku eneo la Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam, ambapo alipigwa risasi sehemu ya makalio wakati akijaribu kuwakimbia polisi kwa kutumia gari la mpenzi wake.Mpenzi huyo (jina linahifadhiwa), alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi ya ubakaji.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana katika wodi ya Hospitali ya Temeke alikolazwa, msichana huyo alisema siku ya tukio alikutana na kijana huyo majira ya saa 8:00 usiku katika baa moja inayoitwa Kindau na kukubaliana kwenda kushiriki tendo la ndoa kwa malipo ya Sh 20,000.
Alisema kutokana na muda huo kuwa usiku sana hawakuweza kwenda katika nyumba ya kulala wageni na badala yake walikwenda eneo la Zakhem na kisha walipaki gari kwenye uchochoro na baadae walianza kubanjua amri ya sita.
Wakiwa kwenye kilele cha mapenzi yao, ghafla walishtukia gari la polisi likiwajia kwa kasi kwa nia ya kuwakamata.
“Tuliagana anilipe elfu ishirini wala hakunibaka kama anavyodai, wao polisi walitukuta tayari tunamaliza lakini kutokana na woga tulikimbia ili tusikamatwe,” alisema msichana huyo.
Alisema wakati wanakimbia kwa kutumia gari la mpenzi wake askari mmoja alifyatua risasi iliyopenya kwenye taa ya gari na kwenda kumjeruhi sehemu ya makalio yake.
“Nilisikia mlio mkubwa wa bunduki, ghafla nilihisi kitu kimeingia mwilini mwangu na kuishiwa nguvu,” alisema kwa uchungu.
Alisema kwa kuona hali hiyo, mpenzi wake alisimamisha gari kwa kujisalimisha na polisi walipowafikia walimtaka mpenzi wake huyo atoe pesa kama malipo ya kitendo chao cha kukutwa wakifanya mapenzi ama sivyo watampeleka kituoni.
Alieleza kuwa mpenzi wake hakuweza kutoa pesa hizo ndipo walipoamua kumpiga na kumpeleka kituo cha polisi cha Mbagala na yeye alifikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, ndugu na jamaa wa mpenzi wake wanapinga hatua ya polisi hao kutumia nguvu kubwa kama watu hao walikuwa watuhumiwa wa ujambazi.
Wakizungumza wakiwa kwenye kituo cha Polisi cha Mbagala kufuatilia hatma ya ndugu yao, ndugu hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini walisema hatua ya polisi kupiga risasi huku wakitambua watu hao sio majambazi ni kitendo cha kinyama.
“Tunachoshangaa ni kwa nini polisi wapige risasi wakati wakijua hawakuwa majambazi ila walikuwa wakifanya mapenzi, hata hilo jalada la kesi walilofungua wanataka kuficha maovu yao na sio vinginevyo,” alisema ndugu mmoja ambaye alijitambulisha kuwa shemeji yake.
Alisema kimsingi tukio hilo lilikwenda katika makubaliano yao na sio ubakaji kama wanavyodai, ila kinachofanyika kwa sasa ni kutaka kumlinda askari mwenzao aliyejeruhi kwa risasi.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, David Misime, alipopigiwa simu kuelezea tukio hilo, alisema kwa sasa hawezi kulizungumza kwa kuwa yupo nje ya Mkoa kikazi.
No comments:
Post a Comment