Friday, March 01, 2013

Mtendaji mkuu TAZARA Bw. Akashambatwa Mbikusita-Lewanika aachia ngazi.



Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) Bw. Akashambatwa Mbikusita-Lewanika,(Pichani) hatimaye ameachia ngazi baada ya kuendesha kampeni kali ya miezi kadhaa kutaka aendelee kuongoza Mamlaka hiyo kwa miaka mingine mitatu.
Hatua hiyo ya kuachia ngazi imekuja baada ya Bodi ya Wakurugenzi na Baraza la Mawaziri la Mamlaka hiyo kuonyesha dhahiri kutotaka Mzambia huyo aendelee na uongozi wa TAZARA kutokana na utendaji wake mbovu na uongozi mbaya uliowabagua wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kwa misingi ya utaifa wao.
Habari za ndani za Mamlaka hiyo zimesema Bw. Akashambatwa ambaye kipindi chake cha uongozi kiliisha tarehe 22 Januari, 2013 kiliongezwa kwa maombi maalum ya Serikali ya Zambia kwamba Serikali hiyo ilihitaji muda mrefu kidogo kumpata mbadala wake, licha ya Serikali ya  Tanzania kutoridhishwa na utendaji wake.
Katika kikao chake cha tarehe 20 Februari, 2013 jijini Lusaka, Zambia, Baraza la Mawaziri lilijadili kwa siri na kwa kirefu suala la mtendaji Mkuu huyo ambaye inasemekana aliombewa tena na Serikali ya Zambia kipindi cha nyongeza, ombi ambalo inadaiwa lilipingwa vikali na ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Taarifa za uhakika ndani ya Wizara ya Uchukuzi zinasema Serikali ya Tanzania haikumtaka Mtendaji Mkuu huyo kwa sababu kadhaa zikiwemo :uwezo mdogo, ubadhirifu, kuchochea ubaguzi kati ya Watanzania na Wazambia, ukaidi na uchochezi. Inadaiwa kuwa Mtendaji Mkuu huyo alizuia kuanzishwa kwa mradi wa usafiri jijini Dar es Salaam bila sababu yoyote ya msngi na kuishia kusambaza taarifa za uongo na uchochezi Zambia na magazeti mbalimbali nchini.
Tarehe 25 Februari, 2013 Gazeti la kila siku la Zambia, Zambia Daily Mail, liliripoti tukio hilo la kuachia ngazi kwa kiongozi huyo ambaye anajulikana sana nchini Zambia kama mfanyabiashara na kiongozi wa kimila (chief),                                              
Gazeti hilo lilinukuu barua ya Bw. Akashambatwa ya tarehe  22 Februari, 2013 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi, Ugavi na Mawasiliano ya Zambia, akielezea kuwa hakuna faida ya kuomba kurefushwa kwa mkataba wake wakati vyombo vikuu vya uongozi vya TAZARA, Bodi ya Wakurugenzi na Baraza la Mawaziri, havionyeshi kumkubali.
Kuondoka kwa Bw. Akashambatwa kwenye uongozi wa TAZARA kunatarajiwa kupokewa na wafanyakazi wa TAZARA kwa nderemo na vifijo.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...