Siku
chache baada ya kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki
duniani, Papa Francis amewashangaza wengi mengi kwa kukataa kuvaa viatu
vya kifahari na msimamo wake kuwekwa wazi kuwa hatavumilia makasisi
watakaotenda uovu.
Papa Francis 1
Tayari,
Papa Francis ameelezwa kuwa kiongozi asiyetaka makuu, mhafidhina na
mtu ambaye hataweza kubadili mengi katika kanisa hilo lenye waumini
bilioni 1.2 duniani.
Katika
siku mbili za uongozi wake, Papa Francis amelithibitisha hilo kwa
kutokea hadharani akiwa amevaa viatu rahisi, vyeusi na kuachana na
vyekundu vya kifahari vilivyopendelewa na mtangulizi wake, Benedict
VXI.
Kutoka Uk 1
Katika
uongozi wake, siku zote Papa Benedict, alivaa viatu vyekundu
vilivyotengenezwa kwa mkono, jambo ambalo Papa Francis anaonekana
kuachana nalo.
Watu
walio karibu naye Papa Francis, wanaeleza kuwa kabla ya kuondoka
Buenos Aires, Argentina kwenda Rome, Kardinali Jorge Mario Bergoglio,
kama alivyojulikana awali, alivaa viatu rahisi vya rangi nyeusi, na
kuwafanya marafiki zake, wakiwamo mapadri kutaka kumnunulia viatu
vingine vipya.
“Siku
ile aliyoondoka mjini Buenos Aires kuelekea Rome kwa ajili ya mkutano
wa uchaguzi wa Papa (conclave), marafiki zake walimpa zawadi ya viatu.
Yeye, siku zote amekuwa akitokea hadharani akiwa amevaa nguo rahisi,
viatu vya kawaida,” walieleza mapadri hao kutoka Amerika Kusini
walipozungumza na Kituo cha Redio Vatican.
Mbele ya makardinali 106
Juzi
Ijumaa alipokutana na makardinali 106, kiongozi huyo mwenye umri wa
miaka 76, licha ya kuonyesha uso wa furaha na kuwatania aliwaonya
makardinali hao kuhusu wajibu wao kama viongozi wa kanisa maeneo
mbalimbali duniani akiwataka kutosahau kuwa hawarudi kwenye ujana.
Katika
ukumbi wa Sala Clementina, ulioko Vatican Papa Francis pia aliwataka
makardinali hao wakiwamo waliomchagua kuwategemea zaidi vijana aliosema
ndio nguzo kuu muhimu ya ustawi wa Kanisa Katoliki, huku aliwashauri
makardinali kusaka njia sahihi ya kueneza Ukristo pande zote za uso wa
dunia katika karne ya 21.
Aidha,
alimsifu mtangulizi wake, Papa Benedict kwa uamuzi wa kijasiri wa
kustaafu, akieleza kuwa ni uamuzi wa busara, wenye kuonyesha ukomavu na
kuwataka wasichoke kuiga matendo mema.
Yaliyomo kitabuni mwake
Kupitia
kitabu, On Earth and Heaven (Duniani na Mbinguni) alichokiandika akiwa
kardinali, Papa Francis alitoa taswira yake kama mtu mwenye dhamira
safi hasa katika masuala ya kusaidia jamii, muumini thabiti anayeamini
katika majadiliano baina ya makundi ya imani tofauti.
Msimamo kuhusu makasisi
Papa
Francis ameonyesha wazi kuchukizwa na matendo ya makasisi (mapadri)
wasio waadilifu, ambao kwa miaka mingi wamelifedhehesha kanisa na
kwamba yeye hakubaliani na wanaoficha maovu ya baadhi ya mapadri
ukiwamo ulawiti.
“Suala
la useja (mapadri kutokuoa) kwamba ndicho chanzo cha ulawiti linaweza
kusahaulika,” anaeleza katika kitabu hicho. “Endapo padri ni mlawiti,
alikuwa hivyo hata kabla ya ukasisi wake. Lakini, hili linapotokea,
lisiangaliwe kwa mtazamo tofauti, lisifichwe.
Kama kiongozi, hutakiwi kutumia madaraka yako kuangamiza maisha ya mwingine.”
Kuhusu
hatua gani atachukua, wakati akiwa Kardinali Bergoglio, alijibu kuwa
hawezi kukubaliana na waovu, lakini alipoulizwa kama askofu angechukua
hatua gani dhidi ya mapadri wa aina hiyo, alijibu,” Nitamfukuza kazi,
kisha kumshtaki, jukumu langu ni kuweka usafi wa kanisa mbele.
“Hili
ni suluhisho kwa matukio kama hayo kama jinsi ilivyopendekezwa
Marekani; lakini si kuwahamisha wakosaji kutoka parokia moja kwenda
nyingine.
“Huu ni upuuzi, kwani hata huko wataendeleza tatizo hilo. Jibu sahihi kwa tatizo hili ni kutowavumilia.”
Katika
kitabu hicho, Papa Francis anazungumzia maisha ya utauwa (usafi wa
moyo), uadilifu na maovu akiweka wazi msimamo wake usio wa mzaha na
kuruhusu mijadala baina ya makundi ya imani tofauti, msimamo ambao
unaweza kupingwa na baadhi ya Wakatoliki wenye msimamo mkali.Kwa maneno
yake, Papa Francis anaonyesha kuwa mtu mwenye akili, anayefikiri
haraka, mjuzi wa mambo, anayechanganya uhafidhina wa kijamii na akiwa
mwenye msimamo mkali wala kutokukubali upuuzi kwa mambo asiyoyapenda au
kuyakubali.
Kiongozi
huyo ameahidi kutumia Jumamosi ya Machi 23 kumtembelea mtangulizi
wake, Papa Benedict katika jumba analoishi huko Castel Gandolf, kusini
mwa Rome na anaeleza kuwa kanisa limepitia nyakati ngumu. “Kumekuwa na
vipindi vingi, majaribu mengi. Kumekuwa na vipindi vigumu, lakini,
kanisa limesimama imara.”
Hata
hivyo, katika misa yake ya kwanza, Alhamisi, Papa Francis alieleza
kuwa kanisa hilo halina budi kwenda na wakati, kukubali mabadiliko.
“Ni
dhahiri kuwa katika historia yake, kanisa limebadilika mno, sioni
sababu za kwa nini tusikubali mabadiliko na kuwa utamaduni wetu wa
sasa,” anaeleza.
Alieleza kuwa mafundisho ya msimu ya Kikatoliki, msimamo kuhusu mashoga, ndoa za jinsia moja, hayawezi kubadilika.
Pia, anaeleza kuwa utoaji mimba ni tatizo la kisayansi zaidi, lakini ambalo haliwezi kukubaliwa na kanisa.
Kuhusu
utandawazi, Papa Francis alieleza kwamba hakubaliani nao kwa kuwa
mfumo huo hauheshimu tamaduni. “Aina ya utandawazi unaofanya vitu vyote
kuwa sawa ni aina ya unyama,” anaeleza akiongeza kwamba tofauti za
kitamaduni hazina budi kudumishwa.
“Hatimaye, utandawazi unageuka njia ya kuwatumikisha wengine,” alisema.