Wanamuziki wote wa kundi la muziki wa
Punk la Pussy Riot la nchini Russia wameachiliwa huru kutoka gerezani
chini ya sheria ya msamaha.
Nadezhda Tolokonnikova aliachiwa huru
kutoka hospitali moja ya gereza lililopo Siberia, wakati mwenzake Maria
Alyokhina aliachiliwa huru Jumatatu huko Nizhny Novgorod.
Wote
wameuita msamaha huo kuwa ni sawa na sarakasi za serikali za kujisafisha
kabla ya kufanyika kwa michezo ya olimpiki ya majira ya joto
itakayofanyika Russia Februari mwakani.
Wanawake hao wanamuziki walifungwa Agosti 2012 baada ya kuimba nyimbo inayokejeli katika kanisa kuu jijini Moscow.
Kitendo chao kilitafsiriwa kama
kumkufuru mungu na wananchi wengi wa Russia lakini kutiwa kwao hatiani
kwa kosa la utukutu ukichochewa na chuki dhidi ya dini ulishutumiwa na
vikundi vya kutetea haki za binadamu, wanaharakati wanaompinga Rais
Vladmir Putin na mataifa ya nje.
Watu wengi wanaotumikia vifungo
wanauona msamaha huo kama jaribio la Rais Putin la kusafisha taswira
yake katika nchi za magharibi na kuiboresha rekodi yake ya haki za
binadamu kabla ya kufanyika kwa michezo ya Olimpiki huko Sochi Februari
2014.
Siku mbili baada ya sheria hiyo ya
msamaha kuanza kutumika, Rais Putin alimsamehe Mikhail Khodorkovsky,
ambaye siku za nyuma alikuwa ni mtu anayeongoza kwa utajiri nchini
Russia na mkosoaji binafsi wa sera za serikali, hatua ambayo pia
ilitafsiriwa kama kuyaridhisha mataifa ya magharibi.