Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Mwigulu Nchemba, amemwonya Spika wa Bunge, Anne Makinda
kuacha kutumia vibaya fedha za Serikali kwa kuwapa posho wabunge kwa
ajili ya kwenda kwenye michezo nje ya nchi.
Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akichangia Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa bidhaa ya mwaka 2013
iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salumu.
Mkuya katika maelezo yake alisema kuwa
kodi hiyo imefutwa kwa laini za simu kwa mtu mmoja mmoja na badala yake
imeongezwa katika kodi kutoka asilimia 14.5 hadi asilimia 17.
Katika mchango wake, mbunge huyo
alionya kuwa kumekuwa na tabia ya kutumia vibaya fedha za umma jambo
alilosema linaanzia ndani ya bunge.
"Naomba tukubaliane katika kubana
matumizi, na hivyo ninakuomba Mheshimiwa Spika tuanze na ofisi yako
achana na kutoa fedha kwa kuwapa wabunge kwa ajili ya kwenda Dubai kwa
burudani,"alisema Nchemba.
Alisema umefika wakati ambao Serikali
inatakiwa kufanya uamuzi wa kutumia fedha katika mambo muhimu ambayo
yanaigusa jamii kuliko mambo ambayo hayana maana. Kwa upande mwingine
aliwalaumu watendaji kuwa wameiangusha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
kwa kushindwa kutoa ushauri na usimamizi mzuri katika makusanyo ya kodi.
Kwa upande wake Mbunge wa kuteuliwa James Mbatia aliinyooshea vidole Serikali kuwa ndiyo iliyovuruga
mchakato mzima wa makusanyo ya kodi ambayo muswada wake ulishapitishwa.
Mbatia alitoa sababu kuwa ndani ya Serikali wamekuwa wakiamua mambo lakini kwenye utekelezaji wake wanagawanyika.
Chanzo:Mwananchi
Kuwa wa kwanza kupata habari kwa ku-Like page Jambo Tz
No comments:
Post a Comment