Wakati Serikali imewasilisha muswada
wa marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Magazeti, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, imepinga marekebisho ya sheria hiyo kwa madai
kuwa hayakufanyiwa tafakuri na utafiti.
Akiwasilisha maoni hayo bungeni jana,
Msemaji wa Kambi hiyo kuhusu Sheria, Tundu Lissu, alisema mapendekezo
hayo yamefikishwa bungeni bila kufanyia tafakuri au utafiti wowote.
"Mwanasheria Mkuu wa Serikali
angefanya utafiti kidogo tu angegundua kwamba kifungu cha 55 hakina na
hakijawahi kuwa na, sababu yoyote ya kuendelea kuwepo katika kanuni ya
adhabu,"alisema .
Alisema hiyo inatokana na kifungu
hicho hicho kutungwa upya, kwa maneno yale yale, kama kifungu cha 31 cha
Sheria ya Magazeti kwamba kifungu hicho hakikupaswa kuwepo kwa sababu,
makosa ambayo kifungu hicho kinafafanua hayako tena kwenye kanuni ya
adhabu na badala yake, yako katika Sheria ya Magazeti.
"Inaelekea katika fasta fasta ya
kupitisha muswada wa Sheria ya Magazeti, kifungu cha 55 kilisahauliwa
katika kanuni ya adhabu wakati vifungu vyote vinavyohusu makosa ya
uchochezi na kashfa ya kijinai vilipohamishiwa katika Sheria ya
Magazeti,"alisema Lissu.