MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SMZ), Maalim Seif
Sharif Hamad, amesema atagombea urais hadi nguvu zitakapomuishia katika
maisha yake.
Mbali na hilo amesema kuwa ataendelea
kutetea nafasi yake ya ukatibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), katika
uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaoanza Novemba Mosi mwaka huu.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alielezea miaka
mitatu ya utendaji wa SMZ katika awamu ya saba ya uongozi wa Serikali
hiyo.
"Nitastaafu pale nitakapoishiwa nguvu,
wengine wanaona Maalim ni kizingiti, aondoke, nasema siondoki ng'o.
Nitaendelea kuwatumikia Wazanzibari na ndiyo ahadi yangu kwao, nasema
nikiwa mzima nitagombea urais na ukatibu mkuu wa chama changu.
"Mchakato wa uchaguzi CUF tayari
umeanza na utafanyika katika matawi yote Novemba mwaka huu, na uchaguzi
mkuu utafanyika mwakani pamoja na mkutano mkuu kati ya Mei na Juni
mwakani na Inshaallah nitagombea tena," alisema Maalim Seif.
Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na
Serikali hiyo ya pamoja inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja
na Chama cha Wananchi (CUF), alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya
Serikali hiyo, moja ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupandisha
bei ya karafuu.