MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SMZ), Maalim Seif
Sharif Hamad, amesema atagombea urais hadi nguvu zitakapomuishia katika
maisha yake.
Mbali na hilo amesema kuwa ataendelea
kutetea nafasi yake ya ukatibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), katika
uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaoanza Novemba Mosi mwaka huu.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alielezea miaka
mitatu ya utendaji wa SMZ katika awamu ya saba ya uongozi wa Serikali
hiyo.
"Nitastaafu pale nitakapoishiwa nguvu,
wengine wanaona Maalim ni kizingiti, aondoke, nasema siondoki ng'o.
Nitaendelea kuwatumikia Wazanzibari na ndiyo ahadi yangu kwao, nasema
nikiwa mzima nitagombea urais na ukatibu mkuu wa chama changu.
"Mchakato wa uchaguzi CUF tayari
umeanza na utafanyika katika matawi yote Novemba mwaka huu, na uchaguzi
mkuu utafanyika mwakani pamoja na mkutano mkuu kati ya Mei na Juni
mwakani na Inshaallah nitagombea tena," alisema Maalim Seif.
Akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa na
Serikali hiyo ya pamoja inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja
na Chama cha Wananchi (CUF), alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya
Serikali hiyo, moja ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kupandisha
bei ya karafuu.
Alisema hali hiyo imewapa wakulima wa
zao hilo ahueni, ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hatua iliyowafanya
wananchi wengi hasa katika vijiji vya Pemba kujenga nyumba bora.
Katika sekta ya utalii, alisema
Serikali inaendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo imekuwa
ikiongezeka, ambapo kwa mwaka jana pekee miradi sita na programu 18
zilianzishwa.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi alisema
SMZ imeweza kuboresha maslahi yao kwa kuongeza mishahara ya wafanyakazi
pamoja na kupandishwa vyeo ambapo pia mwaka 2011/12, Serikali
ilishughulikia suala hilo.
Katiba Mpya
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya,
Maalim Seif alisema, mchakato huo unatokana na dhana na fikra za Rais
Jakaya Kikwete, ambapo kwa busara zake aliona miaka 50 imepita tangu
uhuru, hivyo Watanzania wanahitaji Katiba Mpya ambayo itawashirikisha
wananchi wote.
Alisema suala la kutoa maoni
limekwisha, ambapo aliwataka watu kujadili rasimu ili kama ina mapungufu
yatolewe na si kujadili au kutoa maoni.
"Maoni yalishatolewa, mimi nilitoa
yangu nina uhakika yamezingatiwa, chama changu kimekubaliana na maoni
yale, sasa kwanini nisimuunge mkono Rais, namwomba Mwenyezi Mungu
mchakato huu uishe salama salimini maana wakati mchakato unaendelea
wengine wanapinga Katiba isipite.
"Hata hivyo pamoja na azma njema ya
kuifanya nchi yetu iwe na Katiba Mpya ifikapo mwakani, lazima tukiri
kwamba changamoto nyingi zinaendelea kujitokeza katika suala hili.
"Mtakumbuka mfululizo wa matukio
yaliyojiri hasa baada ya Serikali kuamua kuwasilisha bungeni Muswada wa
Marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, vurugu zilijitokeza bungeni
na kusababisha baadhi ya wabunge wa upinzani wakiwamo viongozi wa kambi
hiyo, kulalamika kutotendewa haki na kuamua kutoka nje, mambo ya ajabu
kabisa.
"Baada ya yote yaliyotokea, Rais bado
akafanya busara ya kukaa meza moja na viongozi wa vyama vyote vya siasa
ili kuyajadili kwa upeo wake yanayolalamikiwa, kati ya madai ya msingi
ni kwamba Zanzibar haikushirikishwa katika sheria hiyo pamoja na mambo
mengine mengi," alisema.
Serikali ya kitaifa
Maalim Seif alisema Serikali ya umoja wa kitaifa itaendelea hadi pale wananchi watakapopiga kura za maoni.
"Wanasiasa wataendelea tu kupiga
kelele, ndiyo, si kila mmoja anataka kuongoza, na inshaalah Serikali hii
itaimarika zaidi ya hapa.
Hata hivyo, Maalim Seif aliwatoa hofu
Wakristo Wakatoliki ambao mapema mwakani wanaadhimisha Jubilei ya miaka
150 ya kanisa hilo tangu kuanzishwa visiwani humo, kuendelea na mchakato
wa sherehe hizo kwani Serikali inawalinda.
Tindikali
Maalim Seif alisema suala la matumizi ya risasi za moto na raia kumwagiwa tindikali, ni suala linalompa wakati mgumu.
"Pamoja na mafanikio hayo, lazima
tukiri kuwa bado tunazo changamoto ambazo tunapaswa tusizifumbie macho,
changamoto ambayo imejitokeza katika siku za hivi karibuni katika nchi
yetu ni suala la vitendo vya hujuma, ikiwamo watu kumwagiwa tindikali,"
alisema.
Elimu
"Zamani darasa moja lilikuwa na
wanafunzi 24 na 30, lakini sasa hivi si ajabu kukuta darasa lina
wanafunzi 80 hadi 100 ambapo inabidi lisimamiwe na walimu wawili, mmoja
anafundisha na mwingine anasimamia nidhamu."
Chanzo: mtanzania
Chanzo: mtanzania
No comments:
Post a Comment