Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni
jana jioni walitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge, baada ya kupuuzwa kwa
mwongozo wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar
itakaposhirikishwa.Wabunge waliotoka bungeni jana yapata saa 12.15 ni
kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi huku Mbunge wa Vunjo na
Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP, Augustine Mrema
akiendelea kubaki ukumbini.
Kitendo cha wabunge hao wa upinzani
kilionekana kuwakera baadhi ya wabunge wa CCM, ambao walisikika
wakiwakejeli kwa kupiga meza huku wakisema: "Kwendeni zenu, tumewazoea."
Wakati wabunge hao wakiondoka, Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikuwa akiwasisitiza wabunge wanaobakia
wawe watulivu, maana kuna usalama wa kutosha ndani ya ukumbi huo.
"Mnaotoka nimewaona wote na mnanijua," alisikika Naibu Spika Ndugai akiwatahadharisha wabunge wa upinzani waliosusa mjadala huo.
Wabunge wa CCM waliendeleza vituko
ambapo baada ya wapinzani kutoka, wabunge Juma Nkamia (Kondoa Kusini),
Hilary Aeshi ( Sumbawanga Mjini) na Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini)
walikwenda kukaa katika viti vya kambi ya upinzani.
Kabla ya kutoka kwa wabunge hao
wabunge wawili kutoka CUF waliomba mwongozo wa Spika, wakitaka muswada
huo kuondolewa ili kuwapa nafasi Wanzanzibar kutoa maoni yao.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed
Mnyaa (CUF) aliomba mwongozo akitaka muswada huo uondolewe, hadi hapo
Wazanzibar watakaposikilizwa.
Alisema kuwa kwa maoni ya Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala wamesikiliza maoni ya wadau wengi, lakini
Zanzibar hawakwenda kuwasikiliza wadau wa eneo hilo.