NI
dhahiri sasa biashara ya kupitisha mizigo katika Bandari ya Dar es
Salaam, imekuwa moto, baada ya Serikali ya Rwanda kupandisha tozo ya
ushuru kutoka dola za Marekani 152 hadi 500 ambazo ni sawa na Sh 800, 000
za Tanzania.
Hali hii
inawezekana kwa namna moja au nyingine, imetokana na mzozo kati ya Rais
Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambao umepelekea
wafanyabiashara wa Rwanda na Uganda kutishia kuacha kupitisha mizigo yao
katika Bandari ya Dar es Salaam.
Itakumbukwa
mzozo huo, umekuja baada ya Rais Kikwete kumshauri Rais Kagame akubali
kukutana na waasi wanaoendelea na vita mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini ushauri huo unaonekana kupokelewa
tofauti na Rais Kagame.
Siri ya
kupandishwa kwa gharama hizo, imefichuka jana baada ya malori mengi ya
wafanyabiashara wa Tanzania kukwama katika mpaka wa Rusumo mkoani
Kagera.
Itakumbukwa
hatua hii, imekuja wiki chache baada ya Chama cha Wasafirishaji wa
Mafuta Tanzania (TATOA), kuitahadharisha Serikali kuwa Rwanda na Uganda,
zimeazimia kwa pamoja kuacha kupitisha mizigo yao kwenye Bandari ya Dar
es Salaam kuanzia Septemba mosi.
Awali,
mamlaka mbalimbali za Serikali mjini Dar es Salaam, zilidai hakuna
uwezekano wa nchi hizo mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), kuacha kuitumia Bandari ya Dar es Salaam zikidai kuwa hizo ni
dhana tu.
Lakini
taarifa zilizolifikia MTANZANIA jana asubuhi kutoka Rusumo, mpakani mwa
Rwanda na Tanzania, zinasema katika kile kinachoonekana kuwa ni dhamira
ya dhati ya kuachana na matumizi ya bandari na barabara za Tanzania,
Mamlaka ya Mapato ya Rwanda (RRA), imepandisha ghafla tozo la barabara
na kusababisha usumbufu mkubwa mpakani.
Chanzo
chetu cha habari kutoka Rusumo, kilisema RRA imepandisha tozo hilo
maarufu kama 'Road Toll' kutoka Dola za Marekani 152 hadi Dola 500 (sawa
na Sh 800,000), ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 200.
"Hali ni
mbaya sana hapa mpakani Rusumo, kwani tangu jana (juzi, Jumapili),
tumekwama hatujui la kufanya baada ya Rwanda kuongeza 'Road Toll' kwa
kiwango kikubwa.
"Foleni
ya magari sasa imeziba kabisa barabara kuanzia Rusumo hadi Benaco na pia
kuelekea barabara nyingine ya kwenda Ngara. Sijui itakuwaje, nadhani ni
lazima kulipa ongezeko hili.
"Kinachostaajabisha
na kudhihirisha wazi kuwa hawa jamaa (Rwanda) sasa hawatutaki ni
kwamba, magari ya namba za Kenya, yanalipa Dola 152 kama kawaida na
kuendelea na safari," mmoja wa madereva wa magari ya mizigo, Maneno
Kagasha, alimkariri dereva mwenzake aliyeko mpakani.
Alisema
magari mengi yaliyokwama Rusumo, yamebeba bidhaa tofauti kupeleka
mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), katika miji ya
Bukavu na Goma iliyo umbali wa kilomita kati ya 300 na 450 kutoka
Rusumo.
Hatua ya
RRA kupandisha Road Toll kwa kiwango kikubwa, inaonekana machoni mwa
wadadisi wa mambo kama njia mojawapo ya kuonyesha hasira za Serikali ya
Rwanda chini ya Rais Paul Kagame dhidi ya Tanzania.
MTANZANIA
liliwasiliana na mamlaka za Serikali kuhusu hilo na kuombwa kupewa muda
wa kuwasiliana na watu wa mpakani kuangalia kwa kina suala hilo.
"Hizi
Road Toll kwa nchi za jumuiya yetu zipo, lakini kupandisha kwa kiwango
kikubwa namna hii, hili ni suala jingine. Hakika ni suala kubwa,"
alisema ofisa mmoja wa TCCIA bila kupenda kutajwa gazetini.
Uhusiano
wa Rwanda na Tanzania kwa muda sasa, umekuwa legelege na huenda hatua
hii ya sasa ni ya kutaka kuzuia magari ya Tanzania yasipeleke bidhaa
huko Goma ambako vita vinaendelea kati ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono
na Rwanda na majeshi ya RDC, yakishirikiana na ya Umoja wa Mataifa
yanayoundwa na bataliani moja ya Tanzania.RC Kagera
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Masawe, alipoulizwa kuhusiana na magari hayo kukwama, alisema hana taarifa kwa sababu muda huo alikuwa safari kutoka Ngara kwenda Bukoba mjini.
"Nipe
muda kidogo, nipo njiani natoka Ngara naelekea mjini, naanza
kulifuatilia suala hili haraka ili kujua ukweli, nitakujulisha," alisema
Kanali mstaafu Masawe.
Juzi
wasomi na wanasiasa mbalimbali, walisema Bandari ya Dar es Salaam ina
matatizo mengi ambayo yanapaswa kutatuliwa ili kurudisha imani kwa
watumiaji.
:CHANZO MTANZAIA
No comments:
Post a Comment