MBUNGE wa
Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, (CHADEMA), amewataka Watanzania
watarajie mapanbano makubwa zaidi bungeni, hata ikibidi ngumi kupigwa,
ili kuleta ustaarabu na kutetea haki ya kidemokrasia katika chombo hicho
cha kutunga sheria.
Ndesamburo
ambaye amekuwa bungeni tangu mwaka 2000, alisema hayo jana katika
mahojiano mafupi na gazeti hili, ofisini kwake Moshi Mjini.
Alisema
nyakati zimebadilika na wabunge wa mwaka 2013 si sawa na wa mwaka 2000;
kwani hawa wa sasa hawako tayari kuona kanuni zinavunjwa waziwazi.
Ndesamburo
alikuwa akizungumzia kauli ya Spika wa Bunge, Anna Makinda, na Naibu
wake, Job Ndugai, ambao wanadai kuwa baadhi ya wabunge wa CHADEMA ni
vinara wa fujo bungeni.
Alisema
siasa za sasa ni za vijana, si za wazee kama ilivyokuwa huko nyuma na
kwamba wazee wanapaswa kuelewa kuwa nyakati zimebadilika.
Alisema
kwamba katika siasa za kuelekea mwaka 2015, CHADEMA ina nafasi kubwa ya
kushinda ili kuwaletea Watanzania maendeleo waliyokosa kwa miaka zaidi
ya 50.
Alisema: “Lazima tujifunze kubadilika, hizi ndizo siasa
za wakati huu. Watu wasidhani vijana hawa wa CHADEMA, hata vijana wa
CCM… maana yake kitu kimoja ambacho nimekiona, kama tunajaribu kufikiria
sasa, watu wasidhani ni CHADEMA… lakini kule ndani mpaka vijana wa CCM
wanafanya vurugu. Ukitazama ile filamu iliyoletwa na TBC ilionyesha
CHADEMA tu haikuonyesha upande wa CCM walioshangilia, haikuonesha
kabisa; jambo ambalo si sahihi.
“Kwa hiyo
watu wajifunze kwenda na wakati. Zamani Bunge lilikuwa limetawaliwa na
wazee. Sasa kuna vijana. Vijana ni tofauti na wazee. Lazima wazee waanze
kujua vijana wanataka nini. Sheria na kanuni zinazoendesha Bunge,
vijana wanazijua, zinapovunjwa ni rahisi kuelewa. Zamani hakuna
aliyekuwa anajali hilo.
“Hizi fujo
ni demokrasia. Bunge linashika hamasa, limekuwa zuri. Wala wasione haya.
Hii ni mwanzo tu, tutaona mengi hata ngumi zitapigwa mle ndani. Ndiyo
ustaarabu, hilo ndilo Bunge. Unaponyimwa haki yako, unataka mtu
afanyeje?”
Katika
Bunge la Februari, Bunge lilitawaliwa na fujo, baada ya Spika wa Bunge,
Anna Makinda, na Naibu Spika, Job Ndugai, kuliendesha Bunge kinyume cha
kanuni na kusababisha kuzomewa na wabunge wa upinzani waliodai Spika na
naibu wake wanapinda kanuni.
Mjadala
mkali ulianza wakati wa kujadili hoja binafsi za mbunge wa Ubungo, John
Mnyika, mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, na Mbunge wa
Kuteuliwa na Rais, James Mbatia. Uongozi wa Bunge uliahirisha shughuli
za Bunge mara kadhaa baada ya hali ya kutoelewana na ubishi mkali
kutokea ndani ya Bunge.
Akizungumzia
hali hiyo, Makinda alinukuliwa akisema, “Hata hivyo, imelazimu
kuahirisha mijadala ya hoja binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya
utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge na hivyo kuamua kwa makusudi
kuanzisha vurugu na hivyo kulifanya Bunge lianze kupoteza heshima yake
ya kibunge.”
Alisema
hoja binafsi za wabunge zinaongozwa na kanuni za Bunge kuanzia kanuni ya
53 hadi 58, na kanuni za majadiliano zinaongozwa na kanuni kuanzia 59
hadi 71 ambazo kwa ujumla wake zikifuatwa kama inavyotakiwa vurugu
haiwezi kutokea bungeni.
Makinda
ambaye alionekana kuzungumza kwa jazba, alisema katika mkutano huu
imeonyesha waziwazi baadhi ya wabunge kwa makusudi na kwa nia ya
kupotosha wananchi wanatumia vibaya kanuni hizo na wakati mwingine
kuwadanganya wananchi ambao kwa bahati mbaya kanuni hizi hawazifahamu.
Ubabe huo
wa Spika na naibu wake ulisababisha kwa mara ya kwanza tangu kumalizika
kwa uchaguzi mkuu wa 2010, wabunge wa vyama vya upinzani kuungana
kumsusa Spika na Naibu Spika, wakipinga hatua yake ya kupindisha hoja
mbalimbali zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani.
Wabunge wa
vyama vya upinzani waliotoka kupinga ubabe wa Spika kinyume cha kanuni
ni wa vyama vya CHADEMA, CUF, UDP, TLP na NCCR-Mageuzi ambao waliungana
kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, kupinga hatua ya Ndugai kuwaburuza
katika kupitisha hoja ya Mbatia.
Hoja hiyo
binafsi iliyoainisha udhaifu katika mfumo wa elimu nchini, iliwasilishwa
na kuibua mjadala mzito bungeni, huku kambi ya upinzani ikikubali hoja
ya Mbatia kutaka kuunda kamati teule wakati wabunge wa CCM wakipinga,
hoja iliyosababisha hadi sasa Wazairi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuunda tume inayotafuja tatizo la kufeli kwa wanafunzi wa mwaka
2012.
SOURCE
TANZANIA DAIMA