Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari
Dar es Salaam jana kuhusu Maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama hicho ya
kuwavua nyazifa Naibu Katibu Mkuu,Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu
Kitila Mkumbo Katikati ni Mwanasheria wa chama hicho,Tundu Lissu na
Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa. PICHA | FIDELIS FELIX
----
TAARIFA
KWA WATANZANIA JUU YA UAMUZI WA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA
MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU KUWAVUA NYADHIFA ZA UONGOZI NAIBU KATIBU
MKUU, MH. ZITTO ZUBERI KABWE NA WENZAKE
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana Ubungo
Plaza, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya tarehe 20
Novemba, 2013 hadi alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba, 2013
imetafakari na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali juu ya hali ya
kisiasa ndani na nje ya Chama chetu ambayo kwa muda mrefu imegubikwa na
tuhuma kubwa na nzito dhidi ya Chama chetu na viongozi wake wakuu, yaani
Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB), na Katibu
Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa. Tuhuma hizi zilikuwa na malengo na athari
ya kuwapaka matope na kuwachafua viongozi wakuu wa Chama na Chama
chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya Chama ambao
hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya
utaratibu wa kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande
vipande na hivyo kuua matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa
kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi na kijamii katika nchi yetu
kwa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Uchunguzi
wa Kamati Kuu umebaini kuwepo kwa mkakati mkubwa wa kutimiza malengo
hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko
2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa
Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne, yaani Naibu Katibu Mkuu na
Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Zitto
Zuberi Kabwe ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia kama ‘MM’ au
‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo ambaye kwenye waraka anajulikana pia
kama M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa
amesimamishwa uongozi, Bwana Samson Mwigamba na ambaye kwenye waraka
anaitwa M3; na mtu mwingine ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana
lakini kwenye waraka anajulikana kama M2 na anatajwa kuwa yuko ‘ukingoni
kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika
Sekretariat ya Chama hapa Makao Makuu.
Kwa
mujibu wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na
M3 na kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya
mwisho na kuanza utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri
kwamba MM au Mhusika Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye
mwenyewe Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata
kata kumfahamu M2. Aidha, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kwamba
yote yaliyoandikwa katika ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ yametoka kwenye
‘Mtandao wa Ushindi’ na hayajabadilishwa.