KAMBI Rasmi ya
Upinzani Bungeni, imeibua ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni tisa katika Ofisi ya
Makamu wa Rais (Mazingira), unaohusisha fedha zilizotolewa na wafadhili kwa
ajili ya miradi ya mazingira katika maeneo ya Dar es Salaam, Bagamoyo, Pangani,
Rufiji na Zanzibar.
Kambi hiyo
imeeleza kushangazwa na hatua ya Serikali kuomba tena kiasi hicho cha fedha
katika bajeti ya mwaka 2016/17, kwa ajili ya kazi hiyo hiyo ambayo fedha zake
zilishatolewa na nchi wahisani ambazo ni Marekani na Ujerumani.
Kwa mujibu wa
kambi hiyo, miradi hiyo miwili ilikumbwa na ufisadi mkubwa ambao ulikuwa
ukiendeshwa baina ya mtumishi mmoja aliyeko katika Ofisi ya Makamu wa Rais
Idara ya Mabadiliko ya Tabianchi akishirikiana na kigogo mmoja aliyekuwa Ikulu
wakati wa utawala wa awamu ya nne. Tangaza biashara yako hapa. Pia like page
yetu ya facebook Jambo Tz. tu-follow instagram
@jambotz.
Taarifa hiyo
ilitolewa bungeni jana na Waziri Kivuli katika Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), Pauline Gekul wakati akiwasilisha taarifa ya kambi hiyo kuhusu
Makadirio ya Mapato na Matumizi katika ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17.
“Mtumishi huyo
wa Serikali alishirikiana na kigogo mmoja aliyekuwa Ikulu wakati wa utawala wa
awamu ya nne katika kutafuna fedha ambazo zilikuwa zimetolewa na
wafadhili,” alisema Gekul.
Kutokana na kashfa hiyo aliitaka Ofisi ya Makamu wa Rais imtake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanyie ukaguzi maalumu (Special Audit) wa miradi hiyo miwili.
“Tunataka CAG akague miradi hii ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi , pamoja na miradi mingine yote iliyosimamiwa na Kitengo cha Mabadiliko ya Tabianchi kilichopo chini ya Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, kwani kuna majipu ya kutumbua.
“Tunaomba Bunge
lisitishe kupitisha maombi ya fedha ya mradi huu hadi ukaguzi maalumu
utakapofanyika kuhusu fedha za mradi ambazo zilikuwa zimetolewa na wafadhili
utakapokamilika,” alisema.
Kuhusu mradi wa
Dar es Salaam pamoja na mambo mengine alisema ulitakiwa kusimamiwa na
Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikisha Jiji la Dar Es Salaam na halmashauri
zake kwa ajili ya kutengeneza baadhi ya miundombinu ya majitaka ya jiji hilo.
Gekul ambaye
pia ni Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), alisema kwa mujibu taarifa ya wizara
hiyo inaonesha kuna matatizo makubwa ikiwamo uchache wa watumishi katika Baraza
la Usimamizi wa Mazingira ambayo imelifanya baraza kushindwa kutimiza majukumu
yake.
“Vilevile
ufinyu wa bajeti ambayo inatengwa na Bunge pia umesababisha baraza kukosa fedha
na badala yake linategemea kujiendesha kwa kutegemea faini na tozo ndizo
zinazotumika kuendesha baraza,”alisema.
Gekuli alisema
kambi hiyo inaishauri Serikali kama kweli ina dhamira ya kutaka uchumi wa viwanda,
ni lazima iongeze bajeti katika wizara hiyo na hasa kwa ajili ya shughuli za
baraza hilo ili liweze kufanya tathimini ya mazingira kabla ujenzi na ufufuaji
wa viwanda husika haujaanza kutekelezwa.
“Pamoja na hilo
pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua Serikali ina mipango gani
endelevu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo kuandaa sera
mahususi na kuwa na sheria ya kusimamia utekelezaji wa sera husika.
“Aidha tunataka
kujua tumejipanga vipi kutekeleza kwa vitendo mikataba yote ya kimataifa ambayo
tumeiridhia inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Gekul. Tangaza
biashara yako hapa. Pia like page yetu ya facebook Jambo
Tz. tu-follow instagram @jambotz.
Na Mtanzania
No comments:
Post a Comment