Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
amesema anashindwa kujitokeza kuzungumzia au kufanya mambo
yanayohusiana na urais kwa kuwa Kamati ya Maadili ya CCM inamfuatilia
kwa karibu.
Alisema hayo jana alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais
Jakaya Kikwete wiki iliyopita akiwa Marekani ambako alielezea mafanikio
na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10.
Kikwete alisema: “Wakati unaingia Ikulu unakuwa na
shauku kubwa pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia
kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani
zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza
nilipoishia.”
Kauli ya Lowassa inakuja ikiwa ni siku chache
baada ya makada wengine wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM kueleza
maoni yao juu ya kauli hiyo ya Rais.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba ameshalieleza gazeti hili kuwa kauli hiyo
inampa hamasa kwa nia yake ya kutaka kuwania urais na kwamba alitangaza
nia hiyo huku akifahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo akisema
kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyomsukuma kuchukua
uamuzi huo. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema:
“Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka.
Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo, kwa hiyo hakuna
sababu ya kuwa na wasiwasi.”
Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema:
“Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa
aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi
yake kama mimi.”
Lowassa hajatangaza wazi nia hiyo zaidi ya kusema
ameshawishika kuwania urais baada ya hivi karibuni, makundi mbalimbali
kufika nyumbani kwake mjini Dodoma kumshawishi achukue fomu kuwania
nafasi hiyo.
Miongoni mwa makundi yaliyojitokeza na kumshawishi
pamoja na kumchangia fedha za kuchukua fomu ya kugombea urais ndani ya
CCM ni pamoja na masheikh kutoka wilayani Bagamoyo, wachungaji wa
makanisa ya Kipentekoste, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na madereva
bodaboda.
Msimamo wake hadi jana
Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa
Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk
Mohamed Mhita nyumbani kwa marehemu Oysterbay jijini Dar es Salaam,
Lowassa alisema: “Muda mwafaka ukifika nitatangaza nia na kuweka
mikakati yangu wazi ili wananchi waijue. Kwa sasa siwezi kusema chochote
kwa sababu ninatazamwa sana na chama. Ninachoweza kusema, siku
nitakayotangaza nia, nitaeleza ni nini nitafanya kukabiliana na
changamoto zote zilizopo Ikulu.
“Ninafahamu kuna changamoto nyingi, lakini siwezi
kusema, subirini siku nitakapotangaza nia, nitaelezea ni kwa namna gani
nitakabiliana na changamoto zilizopo katika ofisi hiyo nyeti nchini.”
Waziri mkuu huyo wa zamani, mmoja kati ya makada wa CCM ambao
wameonyesha nia ya kutaka kumrithi Rais Kikwete katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba na pia ni miongoni mwa makada sita wa chama hicho
waliokuwa wamefungiwa kwa miezi 12 na kamati kuu kwa kufanya shughuli
zinazoashiria kufanya kampeni mapema.
Wana-CCM wengine waliotangaza nia na wanaotajwa
katika kinyang’anyiro hicho ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa
Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja
na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment