Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,
Godfrey Kamwela.
MZEE mwenye umri wa miaka 68, Celestine Mushi, mkazi wa kata ya
Motamburu wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, ameuawa na wananchi
wanaotajwa kukasirishwa na kitendo chake cha kupeleka waganga wa jadi
kijijini kwa lengo la kuifanyia zindiko nyumba yake.
Mushi anadaiwa kuwatoa waganga hao wawili jijini Dar es Salaam na kuwapeleka Rombo kwa kazi hiyo maalumu.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,
Godfrey Kamwela aliyesema mauaji hayo yalitokea juzi saa 2.30 usiku
nyumbani kwa Mushi katika kitongoji cha Mbomai Juu, wakati waganga hao
wakiendelea na zindiko lao.
Kamwela aliwataja wanaodhaniwa ni waganga wa jadi kuwa ni Ashraf
Mjengwa (22) na Peter Mmaka (25), wote wakazi wa Magomeni, Dar es
Salaam. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Alisema waganga hao walifika nyumbani kwa Mushi juzi saa 10 jioni, na
ilipofika saa 11 walianza shughuli ya zindiko na walipomaliza, Mushi
alitaka kuwapeleka katika nyumba ya mkwe wake aitwaye Priscila Hilment,
ili nayo ifanyiwe zindiko.
Kamwela alisema kitendo hicho kilikataliwa na mama mkwe, ambaye
alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi ili wawaondoe waganga hao,
ambapo wananchi walifika na kuwashambulia waganga hao.
Alisema kutokana na tafrani hiyo, raia mmoja alitoa taarifa katika
kituo cha polisi, ambapo polisi walifika eneo la tukio na kufanikiwa
kumwokoa mganga mmoja, Mjengwa, ambapo mwenzake alikimbia na kutokomea
kusikojulikana.
Kamwela alisema ilipofika saa 2 usiku, kundi la wananchi
wasiojulikana idadi yake walirudi nyumbani kwa mzee huyo na kuanza
kumpiga kwa fimbo kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake, na kisha
kuondoka na kumwacha akivuja damu nyingi.
Alisema kutokana na damu kuendelea kuvuja, mtoto wa mzee huyo
alimchukua baba yake na kumpeleka katika kituo cha afya cha Tarakea,
ambapo alifariki dunia kabla ya kupatiwa matibabu na Jeshi la Polisi
limeanza msako wa kuwatafuta wahusika.
Mwanajeshi ajinyonga Wakati hayo yakitokea mkoani Kilimanjaro, Grace
Chilongola anaripoti kutoka Mwanza kuwa, fundi wa magari wa Kikosi cha
Jeshi la Ulinzi la Wananchi namba 512 MTC Nyegezi, jijini Mwanza, Jacob
Mponeja (55) amekutwa amejinyonga chumbani kwake kwa kutumia kamba ya
katani huku akiacha ujumbe.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Joseph Lusungu
tukio hilo lilitokea Aprili mosi mwaka huu majira ya saa moja asubuhi.
Alisema ujumbe huo ulioandikwa kwenye kitabu kidogo kilichokutwa
kwenye eneo la tukio ulisomeka; “Kifo changu kimetokana na mke wangu
kujihusisha na vitendo vya kishirikina, hali iliyosababisha kutaka
kuuawa mara mbili na mtu asilaumiwe kwa kifo changu.”
Alisema kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, ambaye ni mwanafunzi katika
sekondari ya Nyabulogoya, kabla ya tukio la kujinyonga, baba na mama
yake Happy Mabula (45), walikuwa na ugomvi mkubwa.
Kaimu Kamanda huyo alisema katika ugomvi huo mama huyo alikatwa shoka
na mumewe na kwamba alikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando
kwa matibabu na kwamba hali yake sio nzuri.
Alisema katika eneo la tukio kulikutwa shoka lililokuwa na damu
pamoja na kitabu hicho kidogo kilichokuwa na ujumbe ulioandikwa na
marehemu. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment