Taasisi ya Mwalimu Nyerere
imesema kuwa wanaotaka aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba akae kimya kuhusu Katiba Inayopendekezwa
hawana hoja.
Imesema kuwa wanaosema hivyo hasa wale wa chama
tawala (CCM) wanatakiwa kujiuliza kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita
wamefanya nini kuhusu Katiba, ikisisitiza kuwa itaendelea kufanya
midahalo ya kuwaelimisha Watanzania kuhusu mchakato wa Katiba ili
utakapofika wakati wa kura ya maoni waelewe kipi wanatakiwa kukifanya
kwa mustakabali wa taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Joseph Butiku
alisema hayo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam katika mahojiano
maalumu na gazeti hili kuhusu kazi na majukumu ya Taasisi ya Mwalimu
Nyerere tangu ilipoanzishwa hadi sasa. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Butiku alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa
taasisi hiyo ni kufanya utafiti utakaochangia kutatua matatizo
mbalimbali kwa njia ya mazungumzo na amani kama ambavyo Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyokuwa akiamini.
Kauli hiyo ya Butiku inakuja siku chache baada ya
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia,
kukaririwa akisema: “Kadri anavyoendelea kupiga kelele, Jaji Warioba
sasa anatutia wasiwasi kwamba, yale siyo maoni ya wananchi, bali ni
maoni yake. Ndiyo maana anayatetea.”
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM,
Abdallah Bulembo alisema: “Sisi tuna nia njema, Mzee Warioba anataka
kuangamiza nchi hii kwa matakwa yake.”
Kwa upande wake Mbunge wa Mbinga (CCM), John Komba
alisema: “Jaji Warioba ni Shida kutokana na kuendelea kujihusisha na
mchakato huo.”
Pia, Butiku jana alisema: “Tunachokifanya sasa
siyo kuwashawishi Watanzania kukataa au kukubali Katiba Inayopendekezwa
bali kuwaelimisha ili wafahamu kilichomo ndani ya Katiba hiyo, hivyo
sisi sote ni washiriki kama wengine.”
Alisema kuwa midahalo kama ya elimu, uchumi na
siasa imefanyika na sasa Watazania wanasema tunataka ifanyike midahalo
inayohusu Katiba kwa lengo la kujibu maswali na siyo kuwaacha njiapanda.
Akizungumza kwa hisia Butiku ambaye ni kada wa CCM
alisema: “Hili jambo ni la Watazania, hakuna mtu anayetakiwa kutetea
hoja zake. Tunazungumza kuhusu mustakabali wa taifa, hivyo tusianze
kubaguana kama mtu alikuwapo au hakuwapo si hoja: Kama ni hivyo, watu wa
CCM walikuwapo miaka 50, wamefanya nini kuhusu Katiba?”
Aliongeza: “Kama hoja ni kuwa na Katiba Mpya na
hii iliyopo mnaitukuza na kusema hili na lile, Warioba hana kosa
kuendelea kushiriki katika mchakato huu na anashiriki kama raia mwingine
au mshiriki mwingine. Tuwaache Watanzania wawe huru, wasitishwe na mtu
yeyote, wasihongwe na wawe huru kutengeneza Katiba yao.”
Alikifafanua alisema: “Sasa hivi watu wote wa
Serikali, Rais, Makamu wa Rais, mawaziri au mtu yeyote ni washiriki tu
katika mchakato huu, kwani Watanzania bado hawajamkabidhi kiongozi wao
Katiba. Nchi hii ni huru, hivyo tuepuke kuuharibu mchakato huu. Vijana
acheni kuwa makuwadi wa kuhongwa, huo ni uhuni ambao vijana wanatakiwa
kuuepuka.”
Mdahalo
Kuhusu mdahalo uliotakiwa kufanyika kesho alisema
kuwa umeahirishwa hadi baadaye ili kuweka mambo sawa kwa kuongeza watoa
mada na washiriki wa kada mbalimbali kujitokeza kufafanya Katiba
Inayopendekezwa.
“Katiba siyo ya kundi lolote…Tunataka kuhubiri
hicho kwa njia ya amani, Katiba haiweze kutengenezwa na Ukawa pekee yao,
Katiba haiwezi kutengenezwa na CCM pekee yao au ikatengenezwa na
madaktari pekee, bali Katiba inatengenezwa na Watanzania wote.”
“Mimi sasa sio mjumbe wa tume, Warioba siyo mjumbe
wa tume, Rais (Jakaya Kikwete) siyo mjumbe wa tume, mbona walikusanyana
pale Dodoma na kushangilia na kutengeneza utaratibu wa kusema ni nzuri
ni nzuri.”
“Sikiliza mbunge wako, sikiliza rais wako,
sikiliza waziri wako, sikiliza Warioba na sikiliza aliyeaminiwa sasa
hivi wote, kwani sasa hivi watu wote ni wachangiaji tu. Tusiseme kuwa
ulikuwa mjumbe wa tume au mjumbe wa Bunge la Katiba usichangie si
kweli,” alisema Butiku.
Aliongeza: “Nenda kwa Chenge au njoo kwangu
nitakueleza…Utakuwa mtu wa ajabu kama utashindwa kwenda kwa Warioba au
utampinga eti kwa kuwa alikuwa mwenyekiti wa tume, wewe unajua kila kitu
kilichoandikwa humo, unajua historia yake, wao wanajua, mbona
tumewaleta watu kutoka nje na hamuulizi…Mbona Bunge limeleta watu kutoka
nje.”
“Vyama viache Watanzania watengeneze Katiba yao,
Serikali iache Watanzania watengeneze Katiba yao, sisi wote tuwasaidie
Watanzania kutengeneza Katiba yao,” alisema Butiku.
Butiku alisema: “Tusiwalazimishe, tusiwatishe,
tusiwahonge, kwa nini tuwahonge vijana kutengeneza Katiba
yao?...Tuwaache Watanzania watengeneze Katiba iliyo bora kwa manufaa ya
taifa lao.”
Akizungumza kwa upole huku akitumia vitabu
mbalimbali ikiwamo Katiba ya CCM na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977
alisema vyama vya siasa hususan vikubwa ndivyo vinavuruga mchakato huu.
Alisema kitendo cha vyama kuhodhi mchakato huo
kilianza wakati Tume ya Katiba ilipowasilisha Rasimu ya Katiba katika
Bunge Maalumu la Katiba kwa kila upande kuvutia kwake jambo ambalo
limesababisha mchakato huo kufika hapa. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment